NAIROBI, Mahakama Kuu ya Kenya imeamuru kwamba mchakato uliokuwa ukiendelea wenye nia ya kuifanyia marekebisho katiba ya nchi hiyo ya mwaka wa 2010 si halali.
Majaji watano waliokuwa wakisikiliza hoja tisa za kupinga kuendelea kwa mchakato huo, walikubaliana kwa kauli moja kwamba kamati ya BBI iliyoundwa na Rais Uhuru Kenyatta na aliyekuwa hasimu wake wa kisiasa Raila Odinga ilikiuka sheria na katiba ya nchi hiyo.
Aidha, jopo hilo lilifikia makubaliano kwamba rais wa Kenya hana uwezo wa kikatiba wa kuanzisha mchakato wa kutaka kufanya marekebisho ya katiba ya nchi hiyo.
Majaji hao, Prof.Joel Ngugi, George Odunga, Jairus Ngaah, Teresia Matheka na Chacha Mwita, walisema kwamba mchakato huo unakiuka kipengele cha 257 cha katiba ya mwaka wa 2010.
“Ni jukumu la bunge kuanzisha mchakato kama huo na wala sio rais,” alisema mmoja wa majaji hao ambapo aliongeza kwamba, rais anaweza kufunguliwa mashtaka kama raia, hata akiwa madarakani, iwapo atakiuka katiba.
Uamuzi huo, uliogusia masuala mbalimbali, uslisomwa na majaji kadhaa.Jaji Ngugi, mwenyekiti wa jopo hilo alisema, “Ni kinyume cha katiba kwa mswada wa bunge kupendekeza ongezeko la idadi ya majimbo au maeneo wakilishi wa bunge.”
“Rais Uhuru Kenyatta amekiuka sheria kwa kuanzisha au kuzindua mchakato wa kutaka kuifanyia marekebisho ya katiba,”uamuzi huo ulieleza.
Mahakama hiyo pia iliamuru kwamba Tume ya Uchaguzi na Mipaka nchini Kenya (IEBC), haiwezi kushiriki kwenye mchakato wa kuifanyia katiba marekebisho, kwa sababu imekiuka katiba na sheria kwa sababu haijakuwa ikiendelea na mchakato wa mfululizo wa kuwasajili wapiga kura.
More Stories
Dk. Mpango amwakilisha Samia sherehe za Uhuru wa Lesotho
Samia atangaza Tanzania kumuunga mkono Odinga
Tanzania yaongoza kikao maalum cha nishati safi