December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Gereza la Butimba, Mwanza. Picha ya Mtandao

Mahabusu 2, mfungwa wauawa wakitoromaka

Judith Ferdinand na Jovin Mihambi, Mwanza

MAHABUSU wawili watuhumiwa wa makosa ya mauaji na mfungwa aliyekuwa akitumikia adhabu ya kosa la kuhujumu uchumi katika Gereza Kuu la Butimba mkoani Mwanza wamefariki wakati wakijaribu kutoroka gerezani.

Akizungumza jana Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro, alisema tukio hilo lilitokea juzi (Aprili 14, 2020) saa 12.30 jioni
eneo la Gereza Kuu Butimba.

Alisema watuhumiwa Yusuph Benard (34) ambaye ni mahabusu mwenye namba 3444/2016 na Seleman Seif (28) mwenye namba 1177/2017 wanaokabiliwa na kesi za mauaji walijaribu kutoroka kwenye gereza hilo siku hiyo

Alisema baada ya tukio hilo ndipo askari magereza wakishirikiana na
wananchi waliwakimbiza na kufanikiwa kuwakamata. “Wananchi
waliwashambulia kwa kipigo kilichosababisha wapate majeraha na baadaye kufariki wakati wakipelekwa hospitali ya Mkoa wa Mwanza Sekou-Toure kwa ajili ya matibabu,” alisema Kamanda Muliro.

Aidha ACP. Muliro, alimtaja mwingine aliyeuawa katika tukio hilo la
kujaribu kutoroka kuwa ni George Aloyce (34) mfungwa namba 200/2019, aliyekuwa akitumikia adhabu ya miaka 15 baada ya kutiwa hatiani kwenye makosa ya kuhujumu uchumi.

Pia alisema mfungwa huyo alikuwa akitumikia kifungo kingine cha miezi
sita baada ya kutoroka akiwa chini ya ulinzi.

Alisema baada ya kukamatwa katika jaribio hilo la kutoroka tena kwenye gereza hilo la Butimba alihojiwa na askari Polisi na kuwaambia kwamba kama wangefanikiwa wangechukua teksi eneo la Mabatini wilayani Nyamagana ili awapeleke Katoro, mkoani Geita.

Alisema waliposhuka kutoka kwenye gari na kuanza  kuelekea alipo
dereva teksi huyo ghafla mfungwa huyo alianza kukimbia. Kamanda Muliro alisema baada ya mtuhumiwa huyo kuanza kukimbia, ndipo polisi waliokuwa naye waliamuru asimame huku wakipiga risasi juu, lakini hakutii amri.

Aliongeza kwamba baada ya kuona mfungwa huyo hataki kutii amri, ndipo walipomrushia risasi zilizomjeruhi miguuni na kufanikiwa kumkamata na kumpeleka hospitali kwa ajili ya matibabu, lakini baadaye alifariki.

Kamanda Muliro alitoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano na taarifa zinazohusiana wahalifu ili wahusika wakamatwe.