Na Penina Malundo,Timesmajira
MENEJA wa Kituo cha Kuzalisha Umeme wa Maporomoko ya Maji Rusumo,Mhandisi Patrick Lweysa, amesema moja ya changamoto inayowakabili kwa sasa katika kituo hicho ni pamoja na uwepo wa magugu maji amyapo yanapunguza uzalishaji wa umeme.
Magugu maji hayo kwa siku yanafikia kiasi cha tani 10 hadi 15 katika eneo la Intake ambayo sehemu kubwa yanayotoka ziwa Rweru ambalo lipo upande wa nchi ya Rwanda na kuyaleta katika Mto wa Kagera.
Mhandisi Lweysa aliyasema hayo Mei 2,2025 wakati wa ziara ya waandishi wa habari kutoka nchi za Tanzania, Rwanda, Kenya, Uganda, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Burundi kuona namna gani kituo hicho kinavyofanya kazi ya uzalishaji wa umeme tangu kukamilika kwake.
Amesema kutokana na uwepo wa changamoto hiyo tayari wamepata mkandarasi kwa ajili ya kufunga kizuio cha magugu maji hayo(Floating Boom) anayejulikana kwa jina la Water and Power Consultancy Services(WAPCOS)kutoka nchini India.
”Matatizo ya magugu maji yanapokuja yanapunguza sana uzalishaji wa umeme kwa sababu ile Hydraulic head ukiipunguza inakuwa moja kwa moja umepunguza uzalishaji.

”Kama uzalishaji unazalisha katika head ya mita 29 unazalisha megawati 28 kwa unit moja kwa hiyo ikipungua kidogo na uzalishaji unaweza kupungua ukawa hata megawati 22 hilo ndo tatizo kubwa tunalokabiliana nalo,”amesema Mhandisi Lweysa
Aidha, amesema endapo kizuio hicho kikifungwa magugu maji hayo yatakuwa yanaenda upande mmoja ambapo kwa upande wao itakuwa rahisi kuyatoa na kuyaweka upande mwingine wa pili, ambapo wananchi watakuwa wanakuja kuyachukua kwa ajili ya kulishia mifugo kama nguruwe, kuku na kwa ajili ya mbole na kuwa faida kwa jamii inayowazunguka.
Aidha, amesema magugu maji hayo yanapoondolewa uwa wanayaflash na kuelekea chini ziwa victoria ambapo wanapoyaflashi utumia maji ambayo ndiyo yanayotakiwa kwenda kuzalisha umeme.

Amesema hiyo, ndiyo hasara ambayo imewafanya kuweka mkandarasi aweze kuweka kizuia.
”Tunapoondoa magugu eneo la intake lazima kwanza uwasiliane na TANESCO kwa upande wa Tanzania, Kampuni ya Umeme ya Rwanda EUCL na REGIDESO kampuni ya umeme Burundi na kuwaambia labda sasa hivi tunazalisha megawati 28 au 26 tunapunguza hadi megawati 10.
”Kwa hiyo muda wa dakika 30 unakuwa umeleta hasara kwa sababu huo umeme inabidi uwe umeuuza kwa hiyo unapata hasara kwa dakika hizo ambazo ni nyingi, lakini hatuna jinsi ni lazima tuyaflash ili tusiendelee kupata hasara kwa kuzalisha umeme kidogo,”amesema.
Soma zaidi:https://timesmajira.co.tz/mradi-wa-umeme-rusumokufikia-asilimia-99-9/
Mhandisi Lweysa amesema kwa kufunga kizuio hicho wataendelea na kuzalisha umeme kama kawaida bila kupunguza chochote.
Mhandisi Jacob Manyuon Deng Afisa Msimamizi wa Mpango wa Nishati ya Kikanda NELSAP – CU,amesema magugu maji hayo yanatakiwa yasafishwe kila siku ili kuyaruhusu maji yaweze kutembea vizuri na kuzalisha umeme.

”Hii ni kazi endelevu ambapo watu wanaendelea kusafisha hadi hapo mkandarasi atakapoanza kazi ya kuweka kizuio cha magugu maji hayo itaweza kusaidia umeme kuzalishwa kama kawaida,”amesema.

Mradi huo wa kufua umeme unaotokana na maji wa Rusumo, umeanza kuzalisha megawati 80 ambazo zinagawanywa kwa usawa wa megawati 27 kwa nchi ya Tanzania, Rwanda na Burundi na hivyo kuzidi kuimarisha gridi za Taifa za umeme.
Kitengo cha Uratibu wa Mpango wa Utekelezaji wa Mpango wa Utekelezaji wa Maziwa ya Ikweta ya Nile (NELSAP-CU), kinasimamia mradi wa umeme kwa niaba ya Serikali za Burundi, Rwanda, na Tanzania ambao ni wamiliki wa mradi huo.

Mradi huo unawaufaisha zaidi ya watu milioni moja Afrika Mashariki na kukuza shughuli za kiuchumi, maendeleo ya sekta binafsi na uwekezaji katika miundombinu kupitia uboreshaji wa upatikanaji wa umeme katika eneo hilo.
More Stories
Kikundi cha Mwanamke Shujaa chamchangia Fedha ya kuchukua Fomu Rais Samia
Wataalam Maendeleo ya Jamii waaswa kutoruhusu tamaduni potofu
CCM yatoa salam za pole kifo cha Msuya