Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
RAIS John Magufuli, amewaagiza viongozi wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama kuchukua hatua dhidi ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD), Ofisa Usalama wa Wilaya (DSO) na Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya (OCCID) katika Mkoa wa Arusha ambako magunia 143 (sawa na tani 2.5) za bangi yalikamatwa ilihali wao wapo.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo jana Ikulu ya Chamwino, jijini Dodoma mara baada ya kuapisha viongozi aliowateua na kushuhudia kuapishwa kwa wateule wake wengine.
Magunia hayo ya bangi yalikamatwa jijini Arusha kupitia operesheni na aliyekuwa Kaimu Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, James Kaji.
Rais Magufuli amempongeza, Kaji kwa kazi hiyo na kusema ameamua kumthibitisha kushika wadhifa huo kutokana na utendaji wake mzuri.
Rais Magufuli aliwapongeza viongozi wote walioteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali walizopangiwa na amewataka kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia viapo vyao, taratibu na sheria na kushughulikia kero za wananchi, badala ya kuacha kero hizo zikisubiri kushughulikiwa na viongozi wa kitaifa.
Katika hafla hiyo Rais Magufuli, aliwaapisha wakuu wa mikoa miwili, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya mmoja na Katibu Tawala wa Mkoa mmoja.
Mbali na Kaji,Rais Magufuli alimuapisha Kamishna wa Polisi, Thobias Andengenye kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Dkt. Philemon Sengati, Mkuu wa Mkoa Tabora na Mariam Mmbaga kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu.
Aidha, Rais Magufuli alishuhudia kuapishwa kwa Kanali Mathias Kahabi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza (SACP) Ismail Mlawa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Albinus Mgonya kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Wilson Shimo kuwa Mkuu wa Wilaya ya Nyang’wale na Abbas Kayanda kuwa Mkuu wa Wilaya ya Karatu.
Wengine aliowashuhudia wakiapishwa kwao ni Toba Nguvila kuwa Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhandisi Martine Ntemo kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Lazaro Twange kuwa Mkuu wa Wilaya ya Babati, Jamila Kimaro kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mpanda na Salum Kalli kuwa Mkuu wa Wilaya ya Magu.
Hafla ya kuapishwa kwa viongozi hao imehudhuriwa na Wakurugenzi wa Halmashauri walioteuliwa hivi karibuni ambao ni Elias Ng’wanidako (Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya), Anastazia Tutuba (Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Same), Saad Mutambule (Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha), Duncan Thebas (Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala) na Mwailafu Edwin (Mkurugenzi wa Mji wa Nanyamba).
Wengine ni Erica Yegella (Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara), Hassan Hassan (Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero), Kanyala Mahinda (Mkurugenzi Mtendaji wa Mji wa Ifakara) na Waziri Kombo (Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo).
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi, Wakuu wa Mikoa, viongozi wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Makatibu Wakuu na viongozi wa Mkoa wa Dodoma.
More Stories
Serikali ya Kijiji Ilungu yawakatia bima za afya wananchi 1500
TMA kuendelea kufuatilia mifumo yake
Wassira:Waliopora ardhi za vijiji warudishe kwa wananchi