Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam
RAIS John Magufuli, amefichua siri za kutengua uteuzi wa baadhi ya viongozi wa Mkoa wa Arusha wakiongozwa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Mrisho Gambo.
Rais Magufuli, amefichua siri hiyo hivi punde, wakati wa hafla ya kuapishwa viongozi aliowateua iliyofanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam.
Walioapishwa ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Idd Kamanta, Mkuu wa Wilaya ya Monduli, DCP Edward Balele, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Bakari Msulwa, Mkurugenzi wa Kaliua, Jerry Mwaga, Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mjiji, Kenan Kihongosi, na Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, John Pima.
Rais Magufuli amesema, hivi karibuni ilibidi atengue uteuzi karibu viongozi wote wa Mkoa wa Arusha kwa sababu katika kipindi chote cha miaka miwili walikuwa wanagombana tu kila mmoja anajiona ni bosi, huku wakitengenezeana mizengwe.
“Wamefanyakazi zao vizuri, lakini hawakuwa na ushirikiano mzuri,” amesema Rais Magufuli na kutumia nafasi hiyo kuwataka viongozi hao wapya waende wakafanyekazi zao vizuri kama walivyofanya kazi kwenye maeneo mengine.
“Ninachowaomba kafanyeni kazi na wakati mwingine mkaridhike na kile mlichonacho kwa sababu wakati mwingine vijana hawaridhiki na kile wanachokuwa nacho wanasahau kuwa kazi bado zipo nyingi sana,”amesema.
Sababu nyingine ya kuwatumbua viongozi hao ni kuwepo kwa mgogoro wa Kanisa na Shule, amesema kulikuwa na mgogoro na kwamba kulikuwa na maneno ambayo hayakuwa ya kweli na kwamba walikuwa wanataka litafutwe eneo lingine ili ilipwe fidia ya sh. milioni 400 na kwamba mgogoro huo alishaumaliza kuwa wajenge ghorofa.
Pia amesema, kulikuwa na mgogoro wa eneo la msikiti na kwamba kuna kiongozi wa Waislamu amekuwa akiwaambia wenzao waombe hilo eneo, wakati inajulikana tangu zamani kwamba ni eneo la wazi.
“Suala la kutaka wapewe eneo hilo lilianza chini ya uongozi wa Mzee Mwinyi (Ali Hassan), akakataa, likaibuka kipindi cha Mzee Mkapa (Benjamin) akakataa, likaja kipindi cha Mzee Kikwete (Jakaya) akakataa. Kwa hiyo msimamo ni ule ule uliowekwa na viongozi waliotangulia,” amesema Rais Magufuli.
Amesema, tatizo hilo limeletwa na Mkuu wa Mkoa aliyekuwepo (Gambo) kwani amekuwa akizungumza hivi, kwingine anazungumza hivi. “Tusimamie sheria, lile eneo ni la wazi kama wanataka kulitumia, basi walitumie kama kutakuwa na shughuli maalum kama Maulidi, lakini sio viginevyo,” amesema.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa