December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi CCM Rais Dkt.John Magufuli akihutubia wananchi wa Dar es salaam(hawapo pichani) waliojitokeza kwa wingi kwenye uwanja wa Taifa wa Benjamini Mkapa .

Magufuli aahidi kulibadilisha Jiji la Dar kuwa kama Ulaya

Na Penina Malundo,TimesMajira,Online

 

MGOMBEA Urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM )Dkt.John Magufuli amesema miaka mitano ijayo anatarajia kuifanya  Dar es Salaam kuwa jiji la mfano barani Afrika  kwa kuhakikisha  wanaimarisha miundombinu mbalimbali ikiwemo  barabara za Juu (Flyover),barabara za chini ,upanuzi wa bandari pamoja na ukamilishaji wa mradi wa reli kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro.

 

Ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam katika uwanja wa Benjamini Mkapa wakati akiongea na Wana Dar es Salaam katika kampeni yake inayoendelea katika jiji hilo.

 

Dkt.Magufuli amesema  anataka watu watakapokuja jijini Dar es Salaam wajue sio Afrika bali wajue Ulaya kutokana na maendeleo yatakayofanyika ndani ya kipindi hicho cha miaka ijayo.

 

“Jukumu la kufanya  Dar es Salaam  kuwa na maendeleo mnalo nyie la kuamua maendeleo au kuamua kutoendelea,”amesema na kuongeza

 

“Mwaka 2015 tulipoingia madarakani tuliwaambia tutaibadilisha  Dar es Salaam , tutajenga flyover  hakuna mtu aliyeamini,lakini leo hii mnajionea ,”amesema.

 

Amesema jiji hilo litabadilishwa kuwa kama Ulaya,  jiji hilo lilivyokuwa chini ya upinzani alipata  shinda katika  kutekeleza miradi  na wakati mwingine ilikuwa ni vigumu hata kufatilia pesa zimetumikaje.

 

“Ninawaomba mniletee wabunge na madiwani wa CCM ili kulisukuma jiji hili  katika mpango mpya .

 

 “Bado nina moto mkali na Dar es Salaam…mwili wangu unawashawasha kwa ajili ya kuliletea jiji hili maendeleo, katika huduma za afya tumepanga kufanya mabadiliko makubwa sana, kwani Dar es Salaam  ina watu milioni sita ni karibu mikoa mitatu au minne ambapo  mwaka 2030 jiji hili linakadiriwa kuwa watu milioni 10 ndio maana mipango yake inatakiwa ifanywe leo,” ”amesema.

 

Aidha miaka mitano ijayo wamejipanga kuimarisha miundombinu ya usafiri ,kukamilisha miradi ambayo haijakamilika ni pamoja na mradi wa barabara ya Moroco ,Mwenge, Bamaga  Shekilango, Kimara, Kibaha barabara ya Pungu,Kifuru,Mbezi Mwisho hadi Mpiji Magoe.

 

Pia amesema wanatarajia kukamilisha mradi wa pili wa mabasi ya mwendokasi kutoka Kariakoo hadi Mbagala , daraja la Salenda na daraja la juu la gerezani pia kukamilisha miradi ya kimkakati ya upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam pamoja na  ujenzi wa reli ya Dar es Salaam hadi Dodoma.

 

Magufuli amesema sambamba na hayo wamepanga kufanya upanuzi wa barabara ya bandari, TAZARA, uwanja wa ndege, Morocco, hadi Kawe, Makongo, Mbagala Kongowe na kuaanza ujenzi wa awamu ya tatu ya .abasi ya mwendokasi kutoka Barabara ya  Nyerere, Bibi titi hadi Azikiwe na huku awamu ya nne ikiendelea na Barabara ya Maktaba Nyerere, Ali hassan Mwinyi, Samojuma hadi Tegeta .