Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online,Magu
HALMASHAURI ya Wilaya ya Magu mkoani Mwanza imeshauriwa kuainisha shule ambazo ni jumuishi na kuweka mkazo katika mafunzo mahususi kwa walimu ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa watoto wenye mahitaji hayo.
Ushauri huo ulitolewa wilayani Magu na Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwanangu Development Tanzania (MWADETA) Walter Miya,wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo Walimu Elimu maalumu na Maofisa Elimu Kata kutoka shule na kata tano za Halmashauri hiyo ya namna ya kuwahudumia watoto wenye changamoto ya mgongo wazi na kichwa kikubwa yaliyotolewa na taasisi hiyo.

Miya amesema,wamewajengea uwezo walimu na Maofisa Elimu Kata ili kujua namna ya kuongeza ujumuishi kwa watoto katika shule za msingi hususani shule za Serikali ambazo zinapokea watoto wengi pamoja na kuwahudumia watoto wenye changamoto ya mgongo wazi wanapokuwa shuleni, kuwatambua na kuwaainisha katika jamii kuanzia ngazi za mitaa na, wanapoletwa shuleni, waweze kuwahudumia akisisitiza kuwa zoezi hilo ni endelevu.
Hivyo wameishauri Halmashauri ya Wilaya ya Magu kuainisha shule zitakazokuwa jumuishi, kwa kuwa ujumuishi hautawezekana katika kila shule.Ambapo alisema,halmashauri inapaswa kuanza kuainisha shule zinazoweza kutoa elimu jumuishi na kuangalia miundombinu inayofaa kuboreshwa.
Amesema Shule ya Msingi Itumbili, iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Magu, ambayo pia ni ya mahitaji maalumu na ina bweni, inaweza kuangaliwa na kupewa kipaumbele ili watoto wanaotoka mbali waweze kutumia huduma hiyo.
Ofisa Elimu Maalumu Idara ya Elimu Msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu,Mwl.James Mgabo amesema, halmashauri hiyo ina vitengo viwili vikuu vinavyohudumia wanafunzi wenye mahitaji maalumu ambavyo vipo katika shule jumuishi.
Amesema shule hizo ni Shule ya Msingi Wita, yenye wanafunzi 86 wenye aina mbalimbali za ulemavu na Shule ya Msingi Itumbili yenye wanafunzi zaidi 100, ambao wote wapo bweni. Wanafunzi hao wana changamoto mbalimbali, wakiwemo wenye changamoto ya akili, ualbino, wasioona na wenye changamoto za afya ya akili.
Mgabo amesema kati ya shule 112 za msingi zilizopo katika halmashauri hiyo, 46 ni jumuishi, huku wanafunzi wenye changamoto ambazo zinaweza kushughulikiwa katika shule hizo wakiendelea kupata elimu. Alisema halmashauri pia ina wanafunzi 290 wenye mahitaji maalumu katika shule mbalimbali wakiwemo wenye changamoto ya mgongo wazi na kichwa kikubwa katika Shule za Msingi Nyamitilo na Ilungu.

Pia amesema,halmashauri ina walimu 22 wenye taaluma ya elimu maalumu na kwa mwaka huu walimu watatu wapo vyuoni wakiendelea na mafunzo. Hata hivyo, alisema bado kuna changamoto ya uwiano wa walimu na wanafunzi wenye mahitaji maalumu kulingana na aina ya changamoto, hivyo Serikali inapaswa kuendelea kuwaongezea walimu hao.
Ofisa Elimu Kata ya Chabula, Ayubu Bindule amesema,mafunzo hayo yana manufaa na ni muhimu kwao kama wasimamizi wa elimu na sera katika ngazi ya kata, kwa kuwa wakati mwingine hupita mitaani na kuona watoto wenye changamoto ya mgongo wazi na kichwa kikubwa.
Amesema,mafunzo hayo yatamsaidia kuhamasisha jamii na kuwasaidia watoto hao kukua na kuendelea kielimu,kwani katika Kijiji cha Chabula amewahi kuona mtoto mwenye changamoto hiyo akiwa nje ya nyumba, hivyo ataanza kwa kushirikisha jamii na wazazi ili kuhakikisha watoto wenye changamoto hizo wanaibuliwa na kupata elimu.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Itumbili Alice Wang’ombe amesema,shule hiyo ni jumuishi na ina wanafunzi wenye mahitaji maalumu na wasio na mahitaji maalumu ikiwa na jumla ya wanafunzi 1,544, ambapo 103 wana mahitaji maalumu katika makundi matano, yakiwemo wasioona, viziwi, wenye ualbino,afya ya akili na wenye ulemavu wa viungo.
Wang’ombe amesema,shule hiyo pia imewahi kuwa na wanafunzi wenye changamoto ya kichwa kikubwa na mgongo wazi, lakini kabla ya kupata mafunzo hayo walimu hawakuwa na uelewa wa kutosha wa namna ya kuwahudumia. Alisema mmoja wa wanafunzi wenye mgongo wazi aliyemaliza darasa la saba alikuwa akihitaji msaada wa karibu katika kutoa haja, jambo ambalo walimu walikuwa wakilifanya kwa msaada wa wazazi.kwa kutumia “pampers”.
Mwalimu wa Elimu Maalumu wa Shule ya Msingi Itumbili, Anneth Stanislaus, ameiomba Serikali kupitia amesema,vyuoni walimu wanafundishwa kuwahudumia na kuwafundisha watoto wenye uziwi na ulemavu wa viungo, lakini watoto wenye mgongo wazi na kichwa kikubwa wamesahaulika, hivyo Serikali kupitia Sera ya Elimu, hasa katika vyuo vinavyotoa mafunzo ya ualimu wa elimu maalumu iwezeshe walimu kupata taaluma hiyo ili waweze kuwahudumia watoto hao ipasavyo.




More Stories
Watoto waathirika wa moyo, jamii yatakiwa kutambua dalili
STAMICO, FDH Tanzania zapanua fursa kwa watu wenye ulemavu
AUMS yasisitiza Local Content katika Madini