Na Judith Ferdinand,TimesMajira Online,Mwanza
IMEELEZWA kuwa takwimu za afya za mwaka 2017-2019,zinaonyesha ongezeko kubwa la magonjwa yasiyoambikiza kutoka wagonjwa 117,984 hadi 189,081 waliofika na kuhudumiwa kwenye vituo vya tiba katika Mkoa wa Mwanza.
Hivyo wananchi wametakiwa kuendelea kuchukua tahadhari katika nyanja mbalimbali ili kuepuka magonjwa hayo sanjari na kuzingatia lishe bora na kujenga utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara.
Akizungumza wakati wa kilele cha maadhimisho ya wiki ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambikiza yanayoadhimishwa kila mwaka Novemba 14,mkoani Mwanza yalifanyika katika uwanja wa Nyamagana, Mganga Mkuu Mkoa wa Mwanza Dkt.Thomas Rutachunzibwa, amesema ongezeko la magonjwa hayo katika mkoa huo ni sawa na asilimia 60, ambapo kati ya hizo ajali ni asilimia 21.3,magonjwa ya moyo hasa shinikizo la juu la damu asilimia 18.8,matatizo yatokanayo na lishe asilimia 11.7,magonjwa ya akili asilimia 11.3 na kisukari asilimia 9.2.
Dkt.Rutachunzibwa amesema katika siku mbili za maadhimisho hayo jumla ya watu 1261 walipatiwa huduma ya upimaji wa viashiria vya magonjwa yasiyoambikiza kama vile kisukari, shinikizo la damu,uwiano wa uzito na urefu na uchunguzi wa lishe pia wametoa elimu kwa jamii na kuweza kuwafikia zaidi ya wananchi 6,227 huku wakifanikiwa kukusanya chupa 461 za damu.
Amesisitiza wananchi kuwa na tabia ya kuchunguza afya zao hata kama haumwi angalau mara mbili kwa mwaka yani kila baada ya miezi sita kwani magonjwa mengi yasiyoambukiza katika hatua za awali hayana dalili za moja kwa moja na zinaanza kuonekana baada ya ugonjwa kuwa mkubwa mwilini.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Emmanuel Tutuba, amesema wananchi wanapaswa kuendelea kuchukua tahadhari katika nyanja mbalimbali ili kuweza kuepuka magonjwa yasiyoambukiza,kuna umuhimu mkubwa wa watu kuendelea kupata huduma za kupima pamoja na kufanya mazoezi hivyo kama Serikali wanajukumu la kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya kufanikisha huduma hizo.
Tutuba amesema,moja ya mambo yanayochangia kuongezeka kwa magonjwa hayo ni mabadiliko ya mitindo isiyofaa ya maisha ya watu ikiwemo ulaji usiofaa wa vyakula vyenye kiwango kikubwa cha mafuta, sukari,chumvi na ulaji mdogo wa matunda na mbogamboga,kutokufanya mazoezi na matumizi makubwa ya vilevi kama vile pombe na tumbaku.
Naye Ofisa Utekelezaji wa Kampuni ya Huduma za Meli(MSCL),Anthony Stephen akizungumza kwa niaba ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo, amesema wao ni miongoni mwa wadahamini katika maadhimisho hayo na waliguswa kwa vile nao ni sehemu ya jamii pia ili kukuza uchumi na kuboresha zaidi sekta ya usafirishaji hususani wa njia ya maji ni lazima wananchi wawe na afya zilizo bora bila ya kuwa na magonjwa mbalimbali ikiwemo kisukari.
More Stories
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25
Meya awafunda wenyeviti Serikali za Mitaa
Mgeja aipongeza CCM kwa uteuzi Wagombea Urais