January 15, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Magonjwa yasioambukiza bado changamoto duniani

Na Heri Shaaban, Timesmajira Online,Ilala

KATIBU Tawala wa Wilaya ya Ilala Charangwa Selemani ,amesema magonjwa yasioambukiza yamekuwa changamoto duniani ikiwemo Tanzania,ambapo yanakuwa tishio kwa afya ya jamii na kuathiri uchumi wa familia na Taifa kwa ujumla.

Selemani ameyabainisha hayo katika uzinduzi wa mradi wa uchunguzi wa magonjwa yasioambukiza uliofanyika hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana wilayani Ilala.

Amesema uchunguzi wa magonjwa yasioambukiza una faida nyingi ikiwemo kugundua mapema magonjwa haya ili hatua za matibabu na ushauri wa kitaalam ziweze kuchukiliwa kabla ya kuleta madhara.

Huku faida nyingine ya kupima afya mapema ni kupunguza gharama za matibabu ambazo mara nyingi huwa kubwa zaidi endapo ugonjwa utagunduliwa katika hatua za mwisho .

Pia amesema,wanashuhudia uzinduzi wa programu hiyo ya miaka mitatu ya kushughulikia magonjwa yasioambukiza, ambayo itatoa fursa kwa wananchi kupata huduma za afya bure za uchunguzi na ushauri muhimu kuhusiana na jinsi ya kujiepusha na magonjwa hayo.

Charangwa amesema, uchunguzi wa magonjwa yasioambukiza utafanyika bure katika vituo vya afya vinne vilivyochaguliwa, na kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na umuhimu wa kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ,hasa kwa watu wenye umri kuanzia miaka 40 na kuendelea

Hivyo amewataka watendaji wa afya ,jamii na viongozi wa kisiasa kushirikiana ili kuhakikisha huduma za uchunguzi na matibabu zinawafikia watu wengi zaidi.

Kwa upande wake Rais wa Chama cha Wataalam wa afya waliopata mafunzo na ujuzi nchini Korea Kusini (KOFIH Global Alumni KGA )Dkt.Lulu Sakafu,amesema mwaka 2017 chama hicho kilianzishwa nchini Tanzania na kuzinduliwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya wakati huo Dkt.Mpoki Ulisunisya,Balozi wa Korea Kusini nchini Tanzania na Rais wa KOFIH wakati huo.

Dkt Lulu,amesema shughuli hizo zimekuwa zikitekelezwa tangu kuanzishwa kwa KGA mwaka 2017,ikiwemo usimamizi wa vifaa vya kitabibu ,mafunzo ya watumiaji vifaa, ,mafunzo kuhusiana na usalama barabarani kwa ajali ya pikipiki,huduma za kwanza uhamasishaji wa jamii,na mafunzo ya utaratibu za msingi za kuokoa maisha ya wagonjwa mahututi pamoja na tafiti za afya ya akili na magonjwa yasioambukiza.