April 16, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mafunzo ya kuripoti uchaguzi mkuu kutolewa kwa waandishi wa habari

Na Bakari Lulela, Timesmajira Online,Dar

CHAMA cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari Nchini(JOWUTA) kwa kushirikiana na Shirikisho la Kimataifa la Waandishi Duniani(IFJ) na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu(THRDC),wanatarajia kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari nchini ya jinsi ya kuripoti uchaguzi mkuu wakiwa salama.

Mafunzo hayo ambayo yanaratbiwa na JOWUTA katika awamu ya kwanza yanatarajiwa kufanyika katika Kanda tatu za Pwani,Nyanda za Juu Kusini na Kaskazini,ambayo yataenda sambamba na maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ambayo yatafanyika jijini Arusha.

Mwenyekiti wa JOWUTA Taifa, Mussa Juma ametoa taarifa hiyo,baada ya kutembelea makao makuu ya ofisi za THRDC, zilizopo jijini Dar-es-Salaam na kufanya mazungumzo na Mratibu wa Kitaifa wa mtandao huo, Wakili Onesmo Ole Ngurumwa.

Juma amesema, katika mkutano wa waandishi wa habari Afrika uliofanyika nchini Senegal na baadae Rwanda, aliomba IFJ na Shirikisho la Waandishi Afrika(FAJ) kusaidia mafunzo kwa wanahabari Tanzania ili waweze kuripoti uchaguzi kwa haki na salama.Ambapo IFJ ikakubali kugharamia sehemu ya mafunzo.

Hata hivyo amesema kutokana na mafunzo kuhitaji gharama kubwa JOWUTA iliamua kuanza kutafuta wadau wengine wa kushirikiana nao wakiwemo THRDC.

Kwa upande wake,Wakili Onesmo Ole Ngurumwa,amesema THRDC kwa muda sasa imekuwa ikitoa mafunzo mbalimbali kwa waandishi ikiwemo sheria za uchaguzi pamoja na ulinzi na usalama kazini.

“Sisi kama wadau wa kutetea haki za binadamu wakiwepo waandishi wa habari,tutachangia mafunzo haya ili waandishi waweze kuripoti vyema uchaguzi mkuu kwa haki,bila upendeleo lakini wakibaki salama,”amesema.

Awali Katibu Mkuu wa JOWUTA, Seleman Msuya,ametoa wito kwa wadau wengine kusaidia wanahabari kupitia JOWUTA ambayo ina zaidi ya wanachama 400 nchi nzima.