January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Maelfu wayakimbia makazi yao Palma

PALMA, Zaidi ya watu 4,000 wamekimbia huko Palma Kaskazini mwa Msumbiji katika wiki wakiongeza idadi ya wakimbizi kufikia 25,000.

Hayo ni kwa mujibu wa takwimu ziliyokusanywa na Shirika la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa (IOM) ambalo wiki iliyopita limechangia dola milioni 1.2.

Kwa mujibu wa taarifa ya shirika hilo iliyotolewa mjini Pemba nchini Msumbiji, Mkuu wa Kazi wa IOM nchini Msumbiji, Laura Tomm-Bonde alisema, “mamia ya watu wenye mahitaji ya dharura ya kibinadamu wanawasili kila siku kwa miguu, basi na mashua kwa sababu ya ukosefu wa utulivu huko Palma.

“Tunaendelea kutoa msaada wa kuokoa maisha lakini tunahitaji msaada zaidi kusaidia kukuza suluhisho la kudumu kwa maelfu ya familia zilizofurushwa ili waweze kuanza kujenga mustakabali mpya wao na familia zao,”amesema.

Shughuli za misaada ya kibinadamu za IOM Kaskazini mwa Msumbiji zinafadhiliwa na mashirika ya wafadhili, kwa msaada wa mchango wa dola milioni 1.2 kutoka kwa Mfumo wa Ufadhili wa Dharura wa Uhamiaji wa IOM.
Mkurugenzi wa Operesheni na Dharura wa IOM alitarajiwa kuwasili Msumbiji kutathmini zaidi hali hiyo na kuthibitisha kujitolea kwa IOM kusaidia watu wenye uhitaji katika eneo hilo.

Taarifa hiyo ya IOM zaidi kuwa,nusu ya waliokimbia makazi yao wako katika wilaya za Mueda (6,970) na Nangade (6,733) kwenye mpaka wa kaskazini na Tanzania.

Wengine wamehamia Kusini zaidi katika mkoa wa Cabo Delgado, watu 5,000 wamewasili katika Jiji la Pemba, na wengine 3,795 katika wilaya ya Montepuez.

IOM inaendelea kutoa msaada wa kisaikolojia na kijamii kwa mamia ya watu waliofurushwa kutoka Palma, pamoja na huduma ya kwanza ya kisaikolojia, ushauri kwa njia ya kundi na usaidizi wa kibinafsi.

Shirika hilo linasafirisha vitu visivyo vya chakula, NFIs, kuongeza shughuli za kusaidia pamoja na kuyafikia maeneo magumu. Wiki iliyopita , vifaa vilitolewa kwa takribani familia 2,000 zilizofurushwa katika wilaya za Mueda na Montepuez, pamoja na maturubai, blanketi, mavazi, ndoo, madumu na vitu vingine muhimu.

Tangu kuanza kwa mwaka huu wa 2021, IOM imetoa msaada wa moja kwa moja kwa zaidi ya watu 40,000 walioathiriwa na ukosefu wa usalama huko Cabo Delgado nchini Msumbiji.