Na Agnes Alcard,Timesmajira online
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Willium Lukuvi, ameongoza maelfu ya wananchi wa Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, kuaga na kutoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais (Mstaafu), Hayati Cleopa Msuya leo Mei 12, 2025 katika Viwanja vya CD Msuya, Mwanga.
Akizungumza wakati wa kuaga mwili huo, Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda akimuelezea Hayati Msuya enzi za uhai wake amesema, alikuwa kiongozi wa mfano wa kuigwa na aliyependa kusimamia haki na ukweli.
Amesema, Hayati Msuya alikuwa kiongozi aliyependa kusimamia ukweli hata katika nyakati ngumu za kusimamia ukweli “Hayati kiongozi wetu Msuya alipenda kusema ukweli hata katika mambo magumu na kipindi kile sisi wengine tulikuwa tukichota busara kwake kuwa hata siku na sisi tukija kuwa viongozi basi tuyaishi yale mema ambayo yeye alikuwa akiyaishi kama kiongozi”, amesema Pinda.
Pia, waziri Mkuu huyo Mstaafu, amewaomba watanzania kuvishukuru vyombo vya dini zote kwa kutumia muda katikati ya ibada kusisitiza na kuhubiti juu ya amani kwa Taifa pamoja na kuwaombea viongozi ili waweze kuongoza nchi kwa busara na amani.
Akitoa salamu za pole kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, ambaye pia Mlezi wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Rabia Abdallah Hamid, amemuelezea Hayati Msuya kuwa, enzi za uhai wake kuwa moja kati ya ajenda zake ilikuwa ni namna gani wananchi wanaendelea kuhudumiwa na kutumikiwa na viongozi nchini.
Pia ameeleza kuwa, Hayati Msuya katika Wilaya ya Mwanga na Mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla, ameacha maendeleo makubwa ya miradi mbalimbali mkoani Kilimanjaro ikiwa pamoja na elimu, barabara na maji ikiwemo mradi wa maji wa Mwanga uliozindukiwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Hayati Cleopa Msuya, atazikwa kesho mkono Kilimanjaro, wilayani Mwanga katika Kijiji cha Usangi, ambapo mazishi hayo yataongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
More Stories
Serikali Kuboresha Elimu ya Ufundi: Shule 55 Kubadilishwa Kuwa Sekondari za Amali
Serikali kutoa Elimu ya mitaala mipya
Waliopata ufaulu wa juu kidato Cha sita mchepuo wa sayansi kupata ufadhili