Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline, Dar
KAMPENI ya msaada wa sheria ya Mama Samia, maarufu Mama Samia Legal Aid imezinduliwa mkoani Katavi ambapo maelfu ya wananchi wanatarajiwa kunufaika na msaada wa kisheria bure kwa muda wa siku 10.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo mwishoni mwa wiki, Mkuu wa Mkoa huo, Mwanamvua Mrindoko, aliwataka wananchi kujitokeza ili matatizo yao yanayohitaji msaada wa sheria yaweze kutatuliwa.
Uzinduzi wa kampeni hiyo ulifanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Kashaulili vilivyopo mjini Mpanda ambapo Mkuu wa Mkoa aliwataka watendaji watakaohudumia wananchi katika kipindi hicho kutowatoza fedha kwani zoezi hilo litaendeshwa bure.
Mrindoko aliwataka wazazi na walezi wa watoto waliofanyiwa ukatili kushirikiana na wataalamu wa sheria ili haki iweze kutendeka huku akisisitiza kuwa kampeni hiyo inalenga kuimarisha huduma za kisheria hasa kwa waathiriwa wa ukatili wa kijinsia, watoto, na makundi mengine yaliyo katika mazingira magumu.
Alisema matarajio yake ni kuona migogoro mbalimbali ya kisheria kama ya ardhi, ndoa, mirathi, migogoro inayohusiana na ukatili wa kijinsia, migogoro ya kukosa matunzo kwenye familia itakwenda kupungua mkoani humo kwa kiasi kikubwa.
Awali, akitoa maelezo ya Kampeni hiyo, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria Dkt. Franklin Rwezimula alisema lengo kuu la Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ni kulinda na kukuza upatikanaji wa haki kwa watu wote kupitia huduma ya msaada wa kisheria nchini.
Alieleza kuwa kampeni hiyo itahusisha utoaji wa elimu kuhusu haki zinazohusu ardhi, ndoa, mirathi, madai, jinai, na haki za binadamu kwa ujumla.
Alisisitiza kuwa kupitia kampeni hiyo, Serikali inalenga kupunguza migogoro ya kisheria na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu masuala ya sheria kwa njia ya mafunzo na huduma za moja kwa moja.
Aidha, Dkt. Rwezimula aliiomba ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa watoa huduma za msaada wa kisheria ili waweze kuwafikia wananchi kwa wakati.
Naye Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Utawala, Katiba na Sheria Boniface Butondo, aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kwa kuwa msaada huo wa kisheria utawasaidia hasa katika kutatua migogoro iliyosababishwa na sheria kandamizi katika masuala ya mirathi, mashamba pamoja na migogoro ya ardhi.
Butondo alieleza kuwa pamoja na mafanikio yanayopatikana chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, wananchi bado wanapaswa kufahamu haki zao za msingi ili waweze kujilinda na kuchangia katika maendeleo ya nchi.
Alisema elimu ya kisheria ni nyenzo muhimu ya kuwawezesha wananchi kutatua changamoto wanazokumbana nazo katika maisha yao ya kila siku.
Uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, umeleta matumaini mapya kwa wananchi wa Mkoa wa Katavi, huku wengi wakisifu jitihada za Serikali za kupeleka huduma za msaada wa kisheria hadi ngazi za mikoa.
Kampeni hiyo iliyozinduliwa mwaka juzi jijini Dodoma inatarajiwa kuleta matokeo chanya katika kupunguza ukatili, migogoro ya kijamii, na kuimarisha utawala wa sheria nchini.
More Stories
Rais Dkt.Samia asajili timu ndani na nje ya Nchi kukabili Marburg
RUWASA Katavi yasaini mkataba ujenzi bwawa la Nsekwa
Wapanda miti 500,kumbukizi ya kuzaliwa Dkt.Samia