Na Esther Macha, Timesmajira Online, Songwe
MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, mkoani Songwe, wameazimia kutokuwa na imani na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Hanji Godigodi kwa madai ya matumizi mabaya ya madaraka na kukwamisha shughuli za maendeleo.
Uamuzi huo uliafikiwa leo katika kikao cha Baraza la Madiwani la kawaida ambapo kwa pamoja walikubaliana kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo hatoshi kuiongoza halmashauri kutokana mwenendo wake.
Akizungumza katika kikao hicho Diwani wa Kata ya Nyimbili, Tinson Nzunda amesema kuwa miongoni mwa masuala yanayomkabili mkurugenzi huyo ni matumizi mabaya fedha zinazotokana na makusanyo ya Kahawa, Ujenzi wa Stendi ya Vwawa, ujenzi wa Shule ya Msingi Kisimani, ukarabati wa magari ya Halmashauri, kutowalipa fedha kwa wazabuni na lugha chafu kwa watumishi na madiwani.
Nzunda amesema kwa kipindi kirefu Mkurugenzi Godigodi amekuwa kikwazo kwao hali inayosababisha shughuli za maendeleo kukwama hivyo wameamua aondoke ili kupisha viongozi wengine watakao kuwa tayari kuwatumikia wananchi na kuleta maendeleo.
“Madiwani kwa umoja wetu tumeazimia kuanzia leo hatumtaki Mkurugenzi huyu, atupishe kwa sababu amekuwa kikwazo katika shughuli za maendeleo, pia hana lugha nzuri kwa watumishi wenzake hata kwetu pia anatoa lugha za dharau tunaomba aondoke tuletewa Mkurugenzi mwingine,” amesema Nzunda.
Diwani wa Kata ya Magamba, Charles Mbalwa ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Fedha na Mipango, amesema mara kwa mara wamekuwa wakihoji matumizi ya fedha za miradi lakini walipohitaji ushirikiano kutoka kwa mkurugenzi hakutimiza majukumu yake.
Amesema miongoni mwa maeneo waliyokuwa wanatilia mashaka ni pamoja na matumizi ya fedha zitokanazo na kahawa ambapo katika kikao kilichopita walihoji makusanyo ya fedha zitokanazo na zao hilo kutoendana na uhalisia wenyewe wa mavuno kwa wakulima..
Kutokana na hali hiyo walihoji ukusanyaji wa mapato na kubaini ubadhilifu wa fedha ambapo walilazimisha Ofisa Ushirika kuchukuliwa hatua za kinidhamu ikiwemo kusimamishwa kazi baada ya kubaini wizi.
Adha amefafanua kuwa tuhuma nyingine ni gharama za matengenezo ya magari ya Halmashauri ambapo walidai fedha iliandikiwa kwa ajili ya matengenezo ilikuwa kubwa kuliko iliyotumika hivyo wamesema Mkurugenzi ana matumizi mabaya ya fedha.
Diwani wa Kata ya Ichenjezya ,Bahati Mbugi amesema, Mkurugenzi huyo hana ushirikiano mzuri na watumishi wenzake na hata madiwani kutokana na kauli mbaya anazozitoa ikiwemo kutoa lugha zisizofaa na dharau pindi wanapohitaji ufafanuzi wa mambo Fulani.
Diwani wa Viti Maalum Tarafa ya Vwawa, Aida Sanatu ameeleza baraza Baraza kuwa Mkurugenzi amechangia kwa kiasi kikubwa kukwamisha shughuli za maendeleo hivyo hawataki kufanya nae kazi.
Hata hivyo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, George Msyani ameungana na madiwani wenzake kuazimia kumuondoa Mkurugenzi kwa madai hawako tayari kufanya nae kazi kutokana na mwenendo wa tabia zake.
Amesema kwa sasa Halmashauri hiyo ikaimishwe kwa Ofisa Mipango ambaye ataendelea na mujukumu hadi pale watakapotafutiwa Mkurugenzi mwingine.
Akijibu tuhuma hizo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbozi, Hanji Godigodi alikanusha tuhuma hizo na kwamba yeye bado ni Mkurugenzi na ataendelea kuwajibika kama kawaida.
Aidha amesema kuwa tuhuma hizo zilizotolewa na madiwani zinachochewa na chuki na visasi kwa sababu ya kusimamia vizuri matumizi ya fedha na majukumu mengine ya utawala.
Amesema ni mara kadhaa amekuwa akitishiwa maisha yake kwa sababu ya kusimamia ukweli katika masuala ya fedha.
More Stories
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25
Meya awafunda wenyeviti Serikali za Mitaa
Mgeja aipongeza CCM kwa uteuzi Wagombea Urais