March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Madiwani Sikonge watakiwa kwenda na kasi ya Rais Samia

Na Mwandishi Wetu Timesmajira Online-Sikonge

MADIWANI wa Halmasahauri ya Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora wametakiwa kwenda kutumikia wananchi kwa kasi na viwango kama Serikali na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan inavyotaka.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo ambaye ni Diwani wa Kata ya Kiloleli,Andrea Lwambano, mara baada ya kuchaguliwa kuongoza halmashauri hiyo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo 2025-2030.

Amesema kuwa wananchi wana imani na matumaini makubwa kutoka kwa Madiwani wao ambao wote wametokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

‘”Ninawashukuru kwa kunipigia kura zote za ndiyo ili niwe Mwenyekiti wenu, nawaahidi kuwa tutafanya kazi kwa ushirikiano na kudumisha umoja na mshikamano wetu kwa manufaa ya wananchi,”amesema Lwambano.

Amesema Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ameshatoa mwelekeo anataka kila Kiongozi aliyechaguliwa na wananchi akawatumikie kwa moyo wa dhati na kuhakikisha kero zao zote zinatatuliwa.

Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo ambaye ni Diwani wa Kata ya Kitunda, Lucas Gerald,ameahidi kushirikiana na Mwenyekiti na Madiwani wenzake ili kuharakisha maendeleo ya halmashauri hiyo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Thomas Myinga,amewataka Madiwani kuwa karibu na wananchi, kusikiliza kero zao, kuzitafutia ufumbuzi na kuelimisha wananchi umuhimu wa miradi inayotekelezwa na serikali.

Aidha amewataka kusimamia ukusanyaji mapato katika maeneo yao ili kuongeza mapato ya ndani ya halmashauri na kuchochea kasi ya utekelezaji miradi ya maendeleo ndani ya kata zao.