Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online -Rukwa
MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi,mkoani Rukwa,wametakiwa kubadilika kwa kufanya kazi kisasa baada ya kupata mafunzo ya uongozi yaliyotolewa na chuo cha Serikali za mitaa Hombolo.
Hayo yamesemwa Februari 21,2026 na Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa Rukwa Vaileth Shirima,wakati akifunga mafunzo ya tatu kwa Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya Nkasi.

Amesema kuwa mafunzo hayo waliyoyapata yakawaimarishe kiutendaji na kuwa wapya kwa kuongeza nguvu katika kuwahudumia wananchi waliowachagua.
Pia amesema,Madiwani wapya ni wengi ukilinganisha na waliorudi katika awamu hii hivyo anatarajia kuona wote wanakua wamoja na kuhakikisha majukumu yao hayaingiliani na ya watu wengine ili kuondoa migongano inayoweza kuzalisha migogoro isiyokuwa ya lazima.
Kwa upande wake Ofisa Tawala Mwandamizi OWM-TAMISEMI,Mashaka Makuka,amesema imani yake ni kuwa mafunzo hayo waliyoyapata Madiwani hao yatakwenda kuibadili halmashauri kwa kuiwezesha kuwa bora zaidi na kutoa huduma stahiki kwa wananchi.
Amesema,udiwani si cheo cha heshima tu bali wanalo jukumu kubwa zaidi hasa pale wanapokuwa na mawazo chanya katika kuiendeleza halmashauri yao.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo,Richard Maasai,amesema Madiwani wanalo jukumu la kulinda na kutunza rasilimali za halmashauri ili ziwanufaishe wananchi.

Awali Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Nkasi,Vareliana Mwampasi,amewaomba Madiwani hao kushirikiana na watendaji kujenga umoja na maelewano yatakayowasaidia kutekeleza majukumu yao vyema .
Baadhi ya Madiwani wamehaidi kuyatumia mafunzo hayo kuwaimarisha kiutendaji na kuyajua majukumu yao sawa sawa .

More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama