Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Korogwe
MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga Sadick Kallaghe amewataka baadhi ya madiwani waache kuwakataa watumishi, watendaji na wataalamu wa Serikali wanaopelekwa kwenye kata zao.
Amesema wapo madiwani ambao kila mtendaji, mtumishi ama mtaalamu anaepelekwa kwenye kata yake ni mbaya na hafai, hivyo anataka kubadilishiwa mwingine, jambo ambalo linawavunja moyo watumishi hao wa serikali.
Amesema hayo kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo robo ya pili mwaka wa fedha 2023/2024 na kuongeza kuwa Diwani kutaka kubadilishiwa watendaji ama watumishi kila wakati pia ni kuchelewesha utendaji kazi kwenye kata yake.
“Haiwezekeni wewe Diwani kila mtumishi anaeleletwa kwenye kata yako hafai, sasa wewe unataka aletwe nani, kama kila mtumishi kwako hafai,” amesema Kallaghe.
Kwa upande wa Watendaji wakiwemo Wakuu wa Idara na Vitengo, amewataka kuwa makini kwenye kila senti ya fedha ya Serikali kwa kuacha kudokoa, ama sivyo watakutana na rungu la kufukuzwa kazi.
“Mnatakiwa kutekeleza miradi kwa uaminifu kwa kuacha kudokoa fedha za miradi,afadhali kama huwezi kufanya kazi kwa uaminifu kwenye halmashauri hii, uandike barua ya kuachia ngazi kuliko kudokoa fedha ya miradi au fedha ya Serikali, ama sivyo utapata tabu sana,” amesema Kallaghe.
Kallaghe amesema makusanyo ya mapato ya ndani bado yapo chini, lakini amesikiliza utetezi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Goodluck Mwangomango kuwa bado eneo kubwa la ukusanyaji mapato hawajalifikia, mkonge na chai, lakini bado kunahitajika jitihada kukusanya mapato hayo.
Katibu wa CCM Wilaya ya Korogwe Vijijini Safina Nchimbi akizungumza kwenye Baraza hilo, aliwaasa madiwani kumsaidia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kusimamia fedha za miradi ya maendeleo zinazopelekwa kwenye halmashauri, kuona thamani ya fedha inalingana na miradi.
Mkuu wa Wilaya ya Korogwe William Mwakilema amesema Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe ipo chini kimkoa katika makusanyo ya fedha za mapato ya ndani, hivyo nguvu za ziada zinahitajika kukusanya mapato hayo.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Goodluck Mwangomango amesema amepokea maagizo na maelekezo yote yaliyotolewa kwenye kikao hicho, na atayafanyia kazi.
More Stories
Jokate awapa tano vijana UVCCM maandalizi Mkutano Mkuu wa CCM
Watakaokwamisha mapato Kaliua kukiona cha moto
Dkt.Gwajima aagiza kuundwa kamati za ulinzi wa watoto