January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Madiwani Korogwe TC wahakikishiwa maji ya uhakika

Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Korogwe

MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini Handeni Trunk Main (HTM) imewahakikishia Madiwani wa Halmashauri ya Mji Korogwe mkoani Tanga kuwa shida ya maji kwenye mji huo itakoma baada ya Mradi wa Maji Miji 28 kukamilika.

Wametoa hakikisho hilo baada ya baadhi ya madiwani kudai kuwa baadhi ya maeneo ya Mji wa Korogwe yana upungufu wa maji, lakini pia kwa wale wanaotumia maji ya visima virefu hasa Kata ya Bagamoyo, baadhi ya visima vinatoa maji yenye chumvi.

Hayo yamesemwa Novemba 12, 2024 na Mkurugenzi Mtendaji wa HTM Mhandisi Yohana Mgaza kwenye Baraza la Madiwani Halmashauri ya Mji Korogwe, robo ya kwanza, na kuongeza kuwa pamoja na Mradi wa Miji 28, lakini pia kuna mradi mkubwa wa maji kutoka Mto Ndemaha, ambapo linajengwa dakio na kulaza bomba kuu lenye urefu wa kilomita 21 ili kuleta maji Mji wa Korogwe.

Akisoma taarifa hiyo kwa niaba ya Mhandisi Mgaza, Mhandisi wa Usambazaji Maji HTM, Ulinaula Mwasimba amesema, Mradi wa Maji wa kutumia chanzo cha Mto Ndemaha unajengewa tenki la kuhifadhi maji lita milioni mbili eneo la Kwamkole. Kunajengwa nyumba ya maabara na vifaa vyake katika eneo la Kwamkole.

“Katika Mradi wa Maji wa kutumia Mto Ndemaha, pia kunajengwa miundombinu ya kusafisha, kuchuja na kutibu maji (Water Treatment Plant) kwa ajili ya kuhakikisha maji yanawafikia wananchi yakiwa safi na salama, tofauti na ilivyo sasa.

“Lakini pia, utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Miji 28 ambapo Mji wa Korogwe ni moja ya miji itakayonufaika na mradi huo, hadi sasa Mkandarasi yupo eneo la mradi anaendelea na ujenzi katika maeneo mbalimbali ya mradi, ambapo anaendelea na ujenzi wa dakio la maji, ujenzi wa chujio, ulazaji wa mabomba, ambapo mpaka sasa amelaza kilomita 103 za mabomba kati ya kilomita 188, na ujenzi wa matenki manane (8) katika maeneo tofauti”amesema Mhandisi Mgaza.

Mhandisi Mgaza amesema katika mipango ya kuondoa changamoto ya maji kwa mipango ya muda mfupi, ni kutumia vyanzo vya visima virefu vya Mbeza mawe, Mtonga na Kwasemangube kwa ajili ya uzalishaji wa maji ili kuimarisha hali ya huduma ya maji katika Mji wa Korogwe.

“Kuboresha miundombinu ya kusambaza maji kwa kulaza bomba lenye urefu wa kilomita 24.9 katika Mji wa Korogwe. Kuendelea kuongeza mitandao ya mabomba ya mabomba katika maeneo ya Mji wa Korogwe ambayo hayana huduma kabisa ya maji kwa kutegemeana na upatikanaji  wa rasilimali fedha.

“Kubadili dira (mita) za maji ambazo ufanisi wake umepungua, kuendana na upatikanaji wa rasilimali fedha. Kuendelea na ukusanyaji wa Maduhuli kwa watu binafsi na taasisi mbalimbali zinazodaiwa”amesema Mhandisi Mgaza.

Mhandisi Mgaza ni kweli baadhi ya maeneo ya Mji wa Korogwe yana upungufu wa upatikanaji wa  maji hasa kipindi hiki cha kiangazi, na hiyo inatokana na upungufu wa maji katika vyanzo vya Mbeza na Mashindei, hivyo kufanya uzalishaji wa maji kuwa mdogo na kuwa na mgao wa maji katika Mji wa Korogwe.

Mhandisi Mgaza amesema changamoto nyingine ni uwezo mdogo wa kuhifadhi maji ukilinganisha na mahitaji ya maji kwa sasa. Uchakavu wa miundombinu iliyojengwa miaka ya 1950 ambayo haijawahi kufanyiwa ukarabati wowote hasa mabomba ya usambazaji maji katika maeneo ya katikati ya Mji wa Korogwe hasa Mtonga, Masuguru, Manundu Kati, Mbeza, Majengo, Kwamkole, Old Korogwe na Manzese.

“Changamoto nyingine ni ukosefu wa miundombinu ya kusafisha na kuchuja maji, hivyo kufanya maji yanayozalishwa kutokuwa na ubora hasa nyakati za mvua, na madeni makubwa kwa taasisi”amesema Mhandisi Mgaza.