Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Ilemela
Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,wamepitisha rasimu ya bajeti makadirio ya mapato na matumizi ya bilioni 84.3 kwa mwaka wa fedha 2025/26,ikiwa ni ongezeko la asilimia 9.
Akiwasilisha rasimu ya makadirio ya bajeti kwa .Waka wa fedha 2025/26, Januari 30,2025,katika kikao cha Baraza la Madiwami,kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Ilemela,Ummy Wayayu,Mchumi wa Halmashauri hiyo,Helbert Bilia amesema, kati ya fedha hizo makisio ya mapato ya ndani ni bilioni 15.0.
Huku miradi ya maendeleo kutoka Serikali Kuu kwa maana ya ruzuku ni bilioni 9,mishahara bilioni 55.2 na matumizi ya kawaida bilioni 4.3,ambapo wanatarajia kuwa na ajira mpya,promosheni na uteuzi wa Wakuu wa Idara.
“Miradi yote viporo 150 iliyojengwa kwa nguvu za wananchi kila Kata,tunaendakuikamilisha ikiwemo sekta ya elimu msingi miradi 66, sekondari 63, utawala 17,afya na maeneo mengine,”amesema Bilia.
Pia amesema Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela zaidi ya asilimia 76 ya eneo lake ni maji,hivyo bajeti hiyo itaenda kuboresha mialo yao ili chanzo hiki cha uchumi cha mazao ya uvuvi na rasilimali ya maji iwe endelevu.
Ambapo wataboresha maeneo ya mialo ya Igombe,Kirumba na Kayenze ambayo inawaingizia mapato pamoja na kununua boti itakayotumika kudhibiti ukwepaji kodi (ushuru) ziwani, kwani wanaamini siyo kila.mtu anapenda kulipa kodi.
Katika msimu wa bajeti unaoendelea wa 2024/2025, kupitia mapato ya ndani wametoa milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya Kata ya Ilemela kwa ukamilifu.Pia wamenunua vitendea kazi kwa ajili ya barabara ikiwemo greda,kijiko na tipa mbili na kwa sasa umefika moja.
Akizungumzia uwekezaji amesema serikali imetoa fursa kupitia mfumo wa uwekezaji kwa ubia,hivyo kuna maeneo sita wameyatangaza ambayo ni vyanzo vitakavyosaidia kuongeza mapato ya Manispaa na kuiwezesha kujiendesha na kuacha kutengeneza vyanzo vya mapato vilivyozoeleka.
“Eneo la Buzuruga ilipokuwa stendi ya mabasi ni muhimu,tunataka kujenga kitega uchumi cha kibishahara ambacho kitabadilisha mandhari ya hapo pia,nyumba za watumishi zitaboreshwa ili kuongeza mapato ya Halmashauri,”amesema Bilia.
Baadhi ya Madiwani wa Halmashauri hiyo akiwemo Diwani wa Kata ya Pasiansi Rosemary Mayunga,amesema rasimu hiyo ya bajeti imegusa Kata,sekta zote na wananchi,hivyo ikitekelezeka kama ilivyopangwa wananchi watakuwa na imani na Serikali.
“Tumejipanga kufanya mikutano ya hadahara kwenda kuwaelimisha wananchi kwba tumeipitisha,imelenga nini na itafanya nini pamoja na yale ambayo yameisha fanya kwa kipindi cha miaka 10,”.
“Ni bajeti ya kimkakati tunapoelekea katika uchaguzi mkuu,imegusa kila sekta, kata na wananchi ni maeneo machache yanahitaji maboresho.Ikisimamiwa vizuri huko kwa wananchi wetu, ilani itakuwa imetekelezwa kwa viwango,”amesema Dede Swila, Diwani wa Shibula.
Diwani wa Buswelu,Sarah Ng’hwani amesema bajeti hiyo inakidhi vigezo, kazi iliyobaki ni kwa Madiwani kuwaambia wananchi kazi ya kuleta maendeleo inayofanywa na Serikali yao ambapo alishauri zahanati ya Pasiansi ijengewe uzio kutokana na umuhimu wake.
More Stories
TAKUKURU yabaini miradi nane yenye dosari
Ilemela yakusanya bilioni 7, mapato ya ndani
Premium Active Tanzania yapunguza uhaba wa madawati Mlele