March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Madiwani Ilala walia na dampo la Pugu

Na Heri Shaaban,Timesmajiraonline,Ilala

MADIWANI wa Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam watoa kilio chao kutokana na changamoto ya miundombinu ya dampo la Pugu Kinyamwezi siyo rafiki .

Akitoa kilio chake katika kikao cha Baraza la Madiwani Halmashauri hiyo,
Diwani wa kata ya Pugu Imelda Samjela, ameeleza  kuwa Dampo hilo lililopo nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam kuwa mazingira yake siyo rafiki ambapo miundombinu yake hasa wakati wa mvua maji yanajaa mengi katika eneo hilo. 

“Dampo la Pugu Kinyamwezi ni kero kubwa tunaomba Serikali na Mhe Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan asikie kilio cha dampo hili wananchi wanapata shida  liboreshwe wakati wa masika maji yanajaa na kuathiri shughuli zingine”amesema Imelda.

Hata hivyo alitumia fursa hiyo kumpongeza Mkuu wa wilaya Edward Mpogolo kuchukua hatua za haraka katika dampo hilo kutatua baadhi ya changamoto.

Wakati huohuo alizungumzia kero ya Kigogo Fresh kuwa daraja limekatika  linapelekea changamoto Walimu na wanafunzi wanashindwa kwenda shule kutokana na changamoto ya miundombinu kuharibika.

Diwani Imelda aliomba Serikali ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam kuchukua hatua kumaliza changamoto haraka wananchi wafurahie matunda ya Serikali yao.

Meya wa Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam Omary Kumbilamoto amejibu kuhusu  kero ya dampo ambapo amesema  Mkuu wa wilaya Edward Mpogolo ameshachukua hatua za kuanza kutatua kero hiyo huku  akimpongeza kwakuchukua hatua za haraka.

Kuhusu ubovu wa miundombinu ya barabara  Meya Kumbilamoto amesema kuwa hivi karibuni watasaini mkataba wa bilioni 10 kwajili ya kujenga barabara za ndani.

Diwani wa Viti Maalum Wanawake wilaya ya Ilala Semeni Mtoka naye alitoa kilio chake kwa Halmashauri ya jiji akiomba wajenge soko la Majohe kwani  wananchi wa Majohe wanapata shida hawana soko la Serikali.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Gerezani Fatuma Abubakari,alitoa kilio chake kwa Halmashauri ya jiji wasiwe wanabadirisha watumishi wa sekta ya afya badala yake ameshauri watumishi  walioamishwa katika kata warejeshwe.