Judith Ferdinand, Timesmajira Online -Mwanza
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela inatarajia kujenga vyumba vya madarasa 72 na matundu ya vyoo 31,kwa shule za msingi zilizopo ndani ya Halmashauri hiyo,kwa mwaka wa fedha 2026/27,ili kuboresha mazingira ya kujifunza na kufundishia.
Akizungumza na Majira Machi 3,2026,Ofisa Elimu, Vifaa na Takwimu, Divisheni ya Awali na Msingi Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Hellen John,amesema jitihada hizo ni fedha kupitia Serikali Kuu,mradi wa Boost/Programu ya Kutekeleza Elimu kwa Matokeo(EP4R),mapato ya ndani ya Halmashauri pamoja na nguvu za wananchi.
Hellen amesema,halmashauri hiyo ina jumla ya shule za msingi za 166 kati ya hizo za serikali 85 na binafsi 81,mahitaji ya vyumba vya madarasa kwa shule za umma ni 1,897 huku yaliopo ni madarasa 851,hivyo Serikali imeendelea kuboresha miundombinu.
Ambapo kupitia Serikali Kuu imetenga kiasi cha milioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mawili,zaidi ya bilioni 1.25 fedha za mradi wa Boost/EP4R,ambazo zitajenga madarasa 45,ukarabati na umalizia nyumba tano za walimu wa msingi na matundu ya vyoo 23.
Halmashauri kupitia mapato yake ya ndani kwa mwaka wa fedha 2026/27,imepanga kujenga vyumba vya madarasa 25 elimu msingi, matundu ya vyoo nane pia kujenga uzio kwa shule za msingi Kirumba,Ziwani na Songambele zilizopo Kata ya Kirumba.
“Serikali imeendelea kuboresha elimu msingi kila mwaka,ambapo kwa mwaka 2025, Ilemela tulipata ajira mpya za walimu 26.Pia wananchi wanajitahidi kujenga maboma ya vyumba vya madarasa huku Serikali ikileta fedha za umaliziaji,”amesema Hellen.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Bulola, Fredrick Kakinda,amesema shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 1130 kati yao wavulana 556 na wasichana 574,walimu 26 kati yao wakike 23 na wakiume 3.
Huku vyumba vya madarasa tisa, matundu ya vyoo 14 kati yao ya wavulana sita na ya wasichana nane,mahitaji ya madawati 376 yaliopo ni 325 upungufu ni madawati 51 lakini hakuna mwanafunzi anayekaa chini.
Pia amesema,matundu ya vyoo hayatoshelezi kwa upande wa wasichana kwani muongozo wa Serikali ni tundu moja la choo wanafunzi 20 wa kike,hivyo mahitaji ya matundu ya vyoo kwa wanafunzi wa kike ni 28 yaliopo 8 hivyo upungufu 20.
Kwa muongozo wa Serikali tundu la choo kimoja wanafunzi wa kiume 25,hivyo mahitaji kwa watoto wa kiume shuleni hapo ni matundu ya vyoo 22, yaliopo sita upungufu ni matundu ya vyoo 16.
Pia amesema kwa upande wa walimu katika shule hiyo wanajitosheleza kwani muongozo wa Serikali tunasema mwalimu mmoja wastani wa wanafunzi 45.
“Walimu wapo 26 na wanafunzi 1130, ukigawanya unapata wastani wa mwalimu mmoja wanafunzi 43, hivyo tunaziada ya wanafunzi wawili,”amesema Mwalimu Kakinda.
Sanjari na hayo ameiomba Serikali kupitia wahisani mbalimbali kuwasaidia kuwajengea matundu ya vyoo katika shule hiyo,huku halmashauri kupitia mapato ya ndani iwakumbuke kuwajengea matundu ya vyoo ili kukidhi mahitaji na kusaidia wanafunzi kuondokana na hadha ya kuchelewa vipindi darasani baada ya mapumziko.

More Stories
TAMWA yakumbusha jamii kupinga ukatili wa kijinsia kuelekea siku ya wanawake Duniani
Wanawake washauriwa kuchangamkia fursa za uchumi
Aida:Wanawake wakipata haki zote itapunguza migogoro