Na Mwandishi Wetu,Timesmajira Online,Kigoma
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara Octavian Mshiu, amewaambia waandishi wa habari mkoani Kigoma kuwa Mkoa huo umekuwa kinara katika ujenzi wa madaraja kwa kutumia teknolojia ya mawe.
Ujenzi huo wa madaraja hayo umeonesha ufanisi wa hali ya juu katika ubora na urahisi wa kufungua barabara vijijini kutokana na gharama za ujenzi wake kuwa nafuu zaidi.
Mshiu amesema kuwa Bodi hiyo imeamua kutembelea madaraja hayo yanayojengwa kwa teknolojia mbadala ya kutumia mawe ili kuona namna ya kusaidia kuisambaza teknolojia hiyo iweze kutumika kwa wingi zaidi nchini.
Hali hiyo itasaidia kuipunguzia serikali gharama za ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya madaraja pamoja na kufungua barabara za vijijini kwa kasi zaidi.
“Mkoa wa Kigoma kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), umejenga jumla ya madaraja 110 kwa gharama ya bilioni 2.4 kiasi ambacho ni nafuu zaidi tofauti kama yangejengwa kwa nondo na saruji kama tulivyozoea ingegharimu zaidi ya bilioni 11, hivyo madaraja haya yameokoa zaidi ya asilimia 80 ya gharama ambazo zingetumika kwa madaraja ya kawaida,”ameeleza Mshiu na kuongeza kuwa
“Madaraja haya pia yametoa ajira kwa wakazi wa Mkoa wa Kigoma ambapo zaidi ya ajira 500 zilitolewa kwa wazawa ili kutekeleza ujenzi huo, hii ni kwa sababu ujenzi wa madaraja ya mawe unatoa ajira kwa mtu yeyote bila kujali kiwango cha elimu alichonacho,”.
Akitolea mfano daraja la Nyamihanga lililoko Wilaya ya Buhigwe ambako mahojiano haya yamefanyika, Mshiu amesema kuwa daraja hilo lipo hatua za mwisho za ujenzi wake lina urefu wa mita 32 na upana wa mita 6 limegharimu kiasi cha milioni 159 ambapo kati ya hizo milioni 70.3 ni fedha za Mfuko wa Barabara.
Makamu Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Mfuko wa Barabara amefafanua kuwa katika hali ya kawaida daraja hilo la Nyamihanga iwapo lingejengwa kwa mfumo wa zege lingegharimu kiasi cha milioni 780 fedha ambayo ingeweza kugawanywa katika miradi mingine ya huduma za kijamii kama vile afya na elimu.
“Eneo tulilopo linaitwa Kwitanga, tunaambiwa magari hayajawahi kuvuka upande wa pili wa mto Luiche kwenda Muzeze tangu tupate uhuru au tangu dunia hii imeumbwa, lakini kutokana na kazi nzuri inayofanywa na serikali barabara hii itafunguliwa hivi karibuni na magari yataweza kuvuka kutoka upande wa Kwitanga kwenda Muzeze,”ameongeza Mshiu.
Akiongea kwa niaba ya wakazi wa Kwitanga Zuwena Kwilelula ameiomba Serikali kukamilisha kwa haraka ujenzi wa daraja hilo la Nyamihanga ili waweze kunufaika na huduma za kijamii upande wa Muzeze ambako kuna zahanati na mashamba ya maharage lakini pia waweze kusafirisha mazao yao kutoka Muzeze kwenda Kwitanga na baadae kuyapeleka sokoni kwa urahisi.
Awali akiwasilisha taarifa yake mbele ya wajumbe wa bodi, Mhandisi Felician Kavishe kutoka TARURA Mkoa wa Kigoma amesema kuwa TARURA mkoani humo imejenga jumla ya madaraja 110 ambapo madaraja 35 yako Wilaya ya Kigoma, 20 Wilaya ya Kasulu, 6 Wilaya ya Buhigwe, 15 Uvinza, 19 Kibondo na 15 Kakonko
Ameongeza kuwa TARURA Kigoma imetumia kiasi cha milioni 383.32 kutoka Mfuko wa Barabara kwa ajili ya ununuzi wa mawe yaliyotumika katika ujenzi wa madaraja 13 ya mawe mkoani humo.
Wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Barabara wako mkoani Kigoma kujionea jinsi teknolojia mbadala kwenye ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja inavyoweza kuipunguzia serikali gharama za ujenzi na matengenezo ya barabara nchini.
More Stories
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa