December 12, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Madaktari wa Tanzania, Comoro waanza kambi kwa kishindo

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

KAMBI Tiba ya Madaktari Bingwa kutoka Tanzania,iliowekwa nchini Comoro imeanza kwa mwitikio wa wananchi wa nchini humo kijitokeza kupata huduma mbalimbali zinazotolewa kwa ushirikiano na madakatari wazawa katika Kisiwa cha Ngazidja.

Madaktari hao wa Tanzani wametoa huduma za uchunguzi na matibabu katika matatizo ya mifupa,figo na kibofu cha mkojo, mifupa, saratani, moyo na mengineyo ambapo takriban wagonjwa 417 wameandikishwa katika siku ya kwanza.

Akizungumza katika kikao cha tathmini ya uendeshaji wa kambi hiyo inayoratibiwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Comoro na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Kaimu Mkuu wa Msafara, Dkt. Salehe Mwinchete, ameeleza kuwa ushirikiano waliopewa na madaktari wenyeji ni mkubwa na wananchi wa Comoro,wamejitokeza kwa wingi na hilo limewatia moyo kuwa siku zinazofuata hali itakuwa bora zaidi.

Naye Balozi wa Tanzania nchini Comoro amewaeleza madaktari hao kuwa Kambi Tiba hiyo imekuwa kivutio kikubwa na wananchi wengi wana imani kuwa katika kambi zijazo fani nyingine za afya zitaingizwa.

Kambi hiyo inahitimishwa Desemba 4,2024,inashirikisha madaktari bingwa kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Hospitali za Benjamin Mkapa, Hospitali ya Muhimbili, Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (MOI).