December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Madaktari wa Rais Samia waibua makubwa halmashauri 184 nchini

Na mwandishi wetu

MATIBABU ya kibingwa kwenye hospitali 184 ngazi ya halmashauri kupitia mpango kabambe wa Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia yamepunguza mateso na kuokoa maisha ya watu wengi waliokuwa wakisumbuliwa magonjwa ya muda mrefu ikiwemo ugonjwa wa uvimbe wa muda mrefu.

Hayo yamesemwa juzi na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, wakati akitoa taarifa juu ya matibabu ya kibingwa yanayotolewa na Madaktari Bingwa wa Rais Samia kwa waandishi wa habari ofisi ndogo za Wizara ya Afya Jijini Dar es Salaam.

“Tumeshuhudia mawe yakiondolewa kwenye vibofu vya mikojo ikiwemo jiwe la ukubwa wa kilo 1 na gram 200, upasuaji wa Goita, watoto 20 wamefanyia upasuaji wa kurekebisha maumbile ya uume (hypospodiasis repair) ambayo yangeweza kusababisha ulemavu wa kudumu,” alisema Waziri Ummy

Aidha, Waziri Ummy alisema katika zoezi hilo takribani wagonjwa 70,000 wamefikiwa ambapo kati yao, madaktari bingwa wa magonjwa ya ndani waliona wagonjwa 22,057 sawa na aslimia 32 magonjwa ya wanawake na uzazi 18,044 sawa na asilimia 26, watoto 14,466 sawa na asilimia 21 na madaktari bingwa wa upasuaji waliona wagonjwa 10,578 sawa na asilimia 15, ambapo kwa ujumla wateja 4,652 sawa na asilimia saba walipata huduma za upasuaji.

Alisema mikoa 10 iliyoongoza kwa wagonjwa wengi waliojitokeza kuonwa na madaktari bingwa wa Rais Samia ni mkoa wa Tanga wateja 4,410, Mara wagonjwa 3,671, Tabora 3,652, Mtwara 3,540, Mwanza 3,256, Ruvuma 3,253, Mbeya 3,126, Kagera 3,122, Pwani 2,966 pamoja na Manyara wagonjwa 2,964.

“Zaidi ya hayo tumebaini, kati ya watoto 14,466 walioonwa, matatizo ya mfumo wa hewa na moyo yaliongoza kwa kuwa na wagonjwa 2,352 sawa na sawa na asilimia 16, uambukizo wagonjwa 2,091 sawa na asilimia 15, upungufu wa damu au Sickle Cell wagonjwa 1,287 sawa na asilimia na Nimonia wagonjwa 1,030 sawa na asilimia saba,” Alisema Waziri Ummy.