January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Madaktari Bingwa wapiga kambi hospitali ya Rufaa-Kitete

Na. Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Tabora

Zaidi ya Shilingi bilioni 21 zimetolewa ndani ya miaka miwili na Serikali ya Awamu ya sita chini ya Uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan , Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kuboresha huduma za afya kwa Mkoa wa Tabora.

Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora ambaye ni Katibu Tawala wa Mkoa Dkt. John Mboya akiongea na wananchi waliofika kupata huduma za kibingwa kwenye hospitali ya ya rufaa ya Mkoa wa Tabora-Kitete.Huduma za kibingwa zitatolewa kwa siku 5 bila malipo.

Hayo yamesemwa leo na Katibu Tawala wa Mkoa huo Dkt. John Mboya wakati akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tabora kwenye uzinduzi wa huduma za kibingwa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora-Kitete ambapo huduma hizo zitatolewa kwa siku 5 na Madaktari bingwa kutoka hospitali za rufaa za Mikoa ya Amana, Temeke na Tumbi.

“Napenda kuipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya Uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maboresho makubwa ambayo yamefanyika katika mkoa wetu wa Tabora na katika hospitali yetu hii ya rufaa ya Mkoa Tabora-Kitete”.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Honoratha Tutatinisibwa akiongea wakati wa uzinduzi wa huduma za kibingwa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora-Kitete ambapo amesema Tabora ina uhitaji mkubwa wa huduma za kibingwa kwa wananchi wake

“Kwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora- Kitete,Serikali ilitupatia fedha kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wodi ya wazazi, jengo la huduma za uchunguzi (mionzi), jengo la huduma za wagonjwa mahututi (ICU), nyumba ya watumishi pamoja na ukarabati wa jengo kwaajili ya Tiba mtandao”.

Amesema jumla ya fedha kiasi cha shilingi Bilioni 6.6 zimetumika katika ujenzi wa majengo hayo pamoja na vifaa Tiba vipya na vya kisasa vitakavyowekwa, pia mapokezi ya vifaa tiba vya kisasa, ambapo moja kati ya vifaa Tiba hivyo ni CT-SCAN yenye thamani ya shilingi bilion 1.8 kwa ajili ya kuendelea kuboresha huduma kwa wagonjwa.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora-Kitete Dkt. Mark Waziri zaidi ya Madaktari Bingwa 20 wamefika kutoa huduma mbalimbali ambapo itawasaidia wananchi pia kuwajengea uwezo madaktari wa hospitali hiyo pia

Kwa ujio wa Madakatari bingwa hao Katibu Tawala huyo amewataka wananchi wa Mkoa wa Tabora kujitokeza kwa wingi  kuweza kupatiwa huduma za matibabu ya kibingwa  bila malipo ili kuweza kuwapunguzia gharama ambazo awali walikuwa wakizitumia kwa kufuata huduma hizo nje ya mkoa  kwenye hospitali ya Taifa na zile za kanda.

Aidha, amesema ujio wa madaktari hao ni njia ya kujengewa uwezo madaktari  ambao ni waajiriwa katika hospitali  ya Kitete katika swala zima la utoaji wa huduma bora kwa wateja wa mkoa huo.

“Hivyo nitoe wito kwa madaktari wetu waliopo katika hospitali hii ya kitete kushiriki kikamilifu katika zoezi la kuwaona wagonjwa kwa kushirikiana na madaktari bingwa hawa ili watakapo ondoka basi ujuzi na taaluma vibaki kwa madaktari wetu” Amesema Dkt. Mboya.

Wakazi wa Tabora wakisubiri kupatiwa huduma mbalimbali za kibingwa ambayo inatolewa na madaktari kutoka hospitali za rufaa za mikoa ya Amana, Temeke na Tumbi

Naye, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Honoratha Rutatinisibwa amewashukuru Madaktari bingwa hao kwa ujio wao ambao utawasaidia wananchi wa Tabora ambao wangepata rufaa ya kwenda Bugando, KCMC, Muhimbili au benjamin Mkapa.

Dkt. Rutatinisibwa amesema kuwa Mkoa wa Tabora unakabiliwa na uhaba wa madaktari bingwa wa fani mbalimbali ambopo kwa sasa mkoa una madakatari bingwa 7 wakati mahitaji ni madaktari sabini na tano (75) na kuongeza kuwa Mkoa kuna mahitaji makubwa kwa wananchi kupata hduma hizo za Kibingwa.

Mkazi wa Tabora akipatiwa huduma ya Kinywa na Meno na Madaktari Bingwa katika hospitali ya rufaa ya Kitete Mkoani Tabora

Awali Mfadhili wa ujio huo wa madaktari bingwa Bw. Jafary Mnete wa kampuni ya Master Card amesema afya ndio mtaji kwa mwanadamu yeyote hivyo kampuni yao imeona umuhimu wa kuwafikishia huduma hizo wananchi wa Tabora ili kuweza kuwaondolea adha ya kufuata huduma za kibingwa nje ya mkoa huo.

Nao wananchi wa Mkoa wa Tabora wameishukuru Wizara ya Afya kupitia Hospitali ya Rufaa ya Tabora-Kitete kwa kuwafikishia huduma za Kibingwa katika mkoa wao na hivyo kuwasaidia kuwapunguzia gharama za matibabu pamoja na rufaa za kuzifuata huduma hizo nje ya mkoa huo.

Mfadhili wa kambi ya madakatari bingwa Bw. Jafary Mnete kutoka Kampuni ya Master Card akiongea na wakati wa uzinduzi wa huduma za kibingwa.