December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Madaktari Bingwa wa Samia watibia wagonjwa 20,922

*Miongoni mwao watoto ni 1,170, watoa huduma halmashauri 56, kampeni yapungunza changamoto kwa Watanzania kufuata huduma mbali

Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline,Dar

WANANCHI 20,922 wameonwa na kupatiwa matibabu na Madaktari Bingwa wa Rais Samia Suluhu Hassan, katika halmashauri 56 zilizopo kwenye mikoa tisa Tanzania Bara tangu kuzinduliwa kwa kampeni hiyo Mei 6, mwaka huu.

Madaktari Bingwa wa Rais Samia wanatoa huduma za kibingwa kupitia kampeni iliyozinduliwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, mkoani Iringa ambapo inalenga kusogeza huduma hizo karibu na wananchi.

Hayo yamesemwa na Msemaji wa Wizara ya Afya, Englibert Kayombo, alipokuwa akizungumza na Gazeti hili, ambapo kati ya wagonjwa hao, watoto ni 1,170.

Akizungumzia mafanikio ya kampeni hiyo ya madaktari Bingwa wa Rais Samia , Kayombo alisema mpango huu umeonesha uhitaji mkubwa wa wagonjwa walioonwa na wataalam wa afya waliokuwepo katika maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara.

“Kwa sasa madaktari hawa wanatoa huduma katika hospitali za Halmashauri, ambapo lengo halisi ni kufika maeneo ya chini kabisa ili kuwasaidia Watanzania wote.

“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia, inataka kupunguza kama sio kuondoa kabisa changamoto za Watanzania, hivyo kwa kupitia program mbalimbali za Wizara ya Afya, tunaamini kwa kiasi kikubwa itasaidia wananchi katika maeneo yote ambayo madaktari hawa watatoa huduma,”amesema Kayombo.

Aidha, Kayombo amesema mbali na kutoa huduma za afya kwa wagonjwa, pia wataalam hao watatumia ujuzi wao kwa kuwanoa wataalam wa afya katika maeneo watakayopita kwa lengo la kuwasaidia katika utoaji huduma endelevu.

Mikoa ambayo mpaka sasa madaktari bingwa wa Rais Samia wametoa huduma ni pamoja na Iringa, Njombe, Songea, Mbeya, Songwe, Lukwa, Manyara, Singida na Dodoma.

Awali wakati Waziri Ummy anazindua mpango huu, alisema wataalam hao wameangalia maeneo yenye uhitaji mkubwa zaidi kama vile madaktari bingwa wa afya ya uzazi na wanawake, watoto na watoto wachanga.

Wengine ni madaktari bingwa wa upasuaji, madaktari bingwa wa magonjwa ya ndani na madaktari bingwa wa usingizi na ganzi, ambapo madaktari hao kwa pamoja wanafikia 25 wanatoa huduma kwa siku siku za wiki.

Kwa mujibu wa Kayombo, madaktari hao wiki hii wanatoa huduma katika Mkoa wa Arusha, Kilimanjaro na Tanga, itakayoongeza idadi ya mikoa itakayokuwa imenufaika na huduma hiyo ya madaktari bingwa wa Rais Samia.