*Utaandika historia kwa Rais Samia kuwa Rais wa kwanza mwanamke wa Afrika kuhudhuria na kushiriki majadiliano ya Mkutano huo
Na Imma Mbuguni, Timesmajiraonline, Rio de Janeiro, Brazil
MACHO na masikio ya Dunia leo yanaelekezwa nchini Brazil unapofanyika mkutano wa wakuu wa nchi zenye uchumii mkubwa zaidi duniani ujulikanao kama G20 unaoanza leo jijini Rio de Janeiro
Kwenye mkutano huo Rais Samia Suluhu Hassan, anakwenda kuandika historia nyingine ambapo anakuwa Rais wa kwanza kutoka Tanzania na Rais mwanamke wa kwanza kutoka Afrika kuhudhuria na kushiriki majadiliano katika Mkutano huo.
Akizungumza hapa wakati alipokutana na wahariri ambao wameambatana na ujumbe wa Rais Samia jana jijini Rio De Janeiro, nchini Brazil, Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa (DMC) Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Noel Kaganda, alisema mkutano huo ni umuhi kwa nchi ya Tanzania
Rais Dkt Samia atashiriki katika mkutano huo kufuatia mwaliko wa Mwenyekiti wa mkutano huo ambaye pia ni Rais wa Brrazil, Luiz Inácio Lula da Silva.
Tukio hilo muhimu na la kwanza kwa Rais mwanamke kutoka Afrika kuhudhuria majadiliano haya makubwa ya kiuchumi na kisiasa, jambo linaloleta furaha kubwa kwa wanawake na viongozi wa Afrika kwa ujumla.
Mkutano wa mwaka huu wa G20 utakuwa na kaulimbiu inayosema;
“Kujenga Jamii yenye Haki, Usawa, na Maendeleo Endelevu” ambayo inaendana na vipaumbele vya Tanzania, kama ilivyoainishwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 na Dira ya Maendeleo ya 2050.
Balozi Kaganda alisema; “Mkutano huu utaangazia masuala muhimu kama mapambano dhidi ya umaskini na njaa, mabadiliko ya nishati, maendeleo endelevu, na mageuzi ya mifumo ya kiutawala katika taasisi za kimataifa masuala ambayo yanashabihiana na ajenda ya Rais Samia ya kujenga jamii yenye ustawi, haki, na ustahimilivu katika nyanja mbalimbali.”
Ushiriki wa Rais Samia katika mkutano huu unadhihirisha wazi jinsi Tanzania inavyotilia mkazo masuala ya maendeleo endelevu, hususan katika maeneo ya nishati safi na kilimo. Tanzania ina maeneo mengi ya kipaumbele ambayo yatashughulikiwa kwenye majadiliano ya G20, hasa linapokuja suala la mazingira bora ya biashara, usalama wa chakula, na upatikanaji wa nishati safi kwa gharama nafuu.
Kwa upande wa nishati, Tanzania inatarajia kutumia fursa ya mkutano huu kuongeza mtindo wa matumizi ya nishati safi, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa fedha za utekelezaji wa miradi ya nishati safi ya kupikia na usambazaji wa umeme kwa watu milioni 300 barani Afrika.
Hii ni muhimu hasa katika kukabiliana na changamoto za upungufu wa nishati na athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo zinawakumba watu wengi barani Afrika.
Aidha, Tanzania ina nafasi ya kipekee ya kujadili namna bora ya kutumia madini ya nadra (rare earth minerals) kwa ajili ya uzalishaji wa nishati safi, ikiwa ni mbadala wa mafuta ya kisukuku.
Kwa upande wa kilimo, Tanzania ina nia ya kuvutia uwekezaji katika masuala ya usalama wa chakula kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa na mbinu zinazohimili mabadiliko ya hali ya hewa.
Mkutano huu ni fursa ya kuhimiza nchi za G20 kuwekeza zaidi katika kilimo cha kisasa kinachozingatia mazingira na kinachoweza kuhimili changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Tanzania, ikiwa ni moja ya nchi zinazoongoza kwa uzalishaji wa mazao ya chakula na kilimo cha biashara barani Afrika, itatumia fursa hii kuhimiza ushirikiano wa kimataifa ili kuongeza uzalishaji wa chakula na kupambana na njaa, hasa katika maeneo yaliyoathirika zaidi.
Mwaliko wa Tanzania katika mkutano huu ni kielelezo cha mafanikio ya diplomasia ya Tanzania inayoongozwa na Rais Samia.
Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa ikijitahidi sana katika kuimarisha ushirikiano na mataifa mengine, na ushiriki wa Rais Samia katika majukwaa ya kimataifa kama vile Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Madola na Mikutano ya Umoja wa Mataifa, ni mifano hai ya mwelekeo huu.
Rais Samia amekuwa akizungumza kwa niaba ya Watanzania na Waafrika, akisisitiza masuala muhimu kama kilimo, njaa, mabadiliko ya tabianchi, na haki za wanawake. Hii ni ishara ya utayari wa Tanzania kushirikiana na mataifa makubwa duniani katika kutafuta suluhu za changamoto zinazoikabili dunia.
Ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa G20 ni fursa kubwa kwa nchi yetu kutambulika zaidi kimataifa. Nchi za G20 zinachangia zaidi ya asilimia 85 ya Pato la Dunia na asilimia 75 ya biashara ya kimataifa.
Hivyo, kuwa sehemu ya majadiliano haya ni fursa ya kupigania maslahi ya taifa na kuhimiza ushirikiano katika masuala ya maendeleo, biashara, na ulinzi wa mazingira. Ushiriki huu utawezesha Tanzania kufikia fursa mpya za misaada ya kiufundi, mikopo, na uwekezaji, hasa katika miradi ya maendeleo na nishati.
Mkutano wa G20 ni jukwaa muhimu la kimataifa ambapo masuala ya uchumi na maendeleo yanajadiliwa na kuainishwa hatua za utekelezaji.
Ushiriki wa Tanzania katika mkutano huu ni hatua muhimu kwa nchi yetu na kwa bara la Afrika kwa ujumla. Kwa kushirikiana na nchi zenye uchumi mkubwa duniani, Tanzania itapata fursa ya kujadili suluhu za changamoto za kimataifa, ikiwa ni pamoja na umaskini, mabadiliko ya tabianchi, na ukosefu wa ajira. Hii ni fursa ya kufanya kazi na nchi nyingine katika kuleta suluhu za kimaendeleo na kuhamasisha utekelezaji wa miradi inayohitaji ushirikiano wa kimataifa.
Ushiriki wa Rais Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa G20 ni hatua kubwa katika uongozi wa Tanzania katika medani za kimataifa.
Ushiriki huu ni fursa ya kuimarisha diplomasi ya nchi, kufungua milango ya uwekezaji na maendeleo, na kutoa mchango muhimu katika muktadha wa changamoto za kimataifa zinazohitaji majibu ya pamoja.
Bila shaka, matokeo ya mkutano huu yatakuwa na manufaa kwa maendeleo ya Tanzania na nchi za Afrika, na yataweka msingi mzuri wa ushirikiano wa kimataifa kwa ajili ya mustakabali bora wa dunia.
MWIISHO————————–
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakani
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best