May 13, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Machinga Dodoma wampongeza Rais Samia kwa ujenzi wa Soko la Kisasa

▪️Ni soko kubwa la kipekee la Machinga Complex▪️Machinga Wanawake Dodoma wazindua Umoja wao

▪️RC Senyamule ataka Jiji kuongeza maeneo ya kufanyia biashara

▪️Mbunge Mavunde awataka Machinga Dodoma kuchangamkia Mkopo wa Bilioni 7 za Jiji Dodoma

Na Mwandishi wetu, Timesmajira

Umoja wa Wanawake Machinga Dodoma(UWAMADO) wamempongeza Rais Dkt. Samia Hassan kwa ujenzi wa soko la kisasa la Machinga Complex na miundombinu ya kisasa ya soko hilo ambalo ni la kipekee nchini.

Hayo yamesemwa jana wakati wa uzinduzi wa chama cha UWAMADO uliofanyika kwenye eneo la soko la Machinga Complex kwa kuzinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule

Akisoma Risala Katibu wa UWAMADO,Mariam Kajembe amesema umoja huo umelenga kuwaleta wanawake Machinga pamoja ili kujijenga na kujiimarisha uchumi.

Aidha pia UWAMADO umempongeza Rais Dkt. Samia Hassan kwa ujenzi wa Soko la Machinga Complex ambalo limesaidia kuwaleta pamoja wafanyabiashara wengi wadogo pamoja ambao awali hawakuwa katika maeneo rasmi na hivyo kuwafanya kutokuwa rasmi.

Akitoa hotuba yake,Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amewapongeza UWAMADO kwa kuamua kuanzisha umoja wao ambao utawasaidia kujiendeleza zaidi na kujiimarisha kiuchumi.

“Jambo hili la kuanzisha umoja ni jambo jema,hakikisheni umoja unafikia malengo mliyokusudia Rais kawajengea soko kubwa na zuri,soko hili liwe kichocheo cha ukuaji wenu kimtaji na kibiashara.

Niwatake Uongozi wa Jiji la Dodoma kuendelea kubuni na kuanzisha maeneo mapya ya kuwapanga vizuri wafanyabiashara wadogo wa Dodoma”Alisema Senyamule

Akitoa salamu zake Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini,Anthony Mavunde amewapongeza UWAMADO kwa kuona umuhimu wa kukaa pamoja kujiinua kiuchumi na kuwataka kuchangamkia fursa ya mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Jiji ambayo kiasi cha Shilingi Bilioni 7 kimetengwa kwa ajili ya kuwawezesha wakina mama,vijana na watu wenye ulemavu.