Na Esther Macha, Timesmajira Online Mbeya
MACHIFU wa Wilaya ya Mbeya wameomba fursa ya kukutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt Samia Suluhu Hassan,kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yenye maslahi mapana kwa Taifa, ikiwemo kukemea matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea Oktoba 29, 2025.
Ombi hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Machifu Wilaya ya Mbeya, Chifu Soja Masoko Desemba 20, 2025, wakati wa Mkutano maalum wa kuombea Taifa na viongozi wake, ulioandaliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini.
“Tunaishukuru Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya chini ya Mkurugenzi Mtendaji,Erica Yegella, pamoja na Mbunge wa Mbeya Vijijini kwa kuhakikisha mkutano huu unafanyika. Lengo lake ni kuliombea Taifa letu amani na utulivu,” amesema Chifu Masoko.
Ombi la Mikopo kwa Machifu

Katika hatua nyingine, Chifu Masoko ameomba machifu wapatiwe mikopo ili kuwawezesha kujikwamua kiuchumi na kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali na biashara mbalimbali, jambo litakalowaongezea uwezo wa kuchangia maendeleo ya jamii zao.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya,Erica Yegella amewasihi machifu kuendelea kuliombea Taifa ili kudumisha amani na mshikamano.
“Ndugu zangu machifu, tunaomba muendelee kuliombea Taifa letu ili amani iendelee kutawala. Nyie ni watu muhimu katika jamii na Taifa kwa ujumla, hivyo tunaendelea kuwathamini na kuwatumia,” alisema.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini, Patali Shida amewapongeza machifu kwa kuandaa kikao hicho na kueleza dhamira yake ya kuona wananchi wa Mbeya Vijijini wanakuwa kitu kimoja chenye mshikamano.
Katika kuhitimisha mkutano huo, machifu walifanya dua maalum kuwaombea viongozi hao wawili pamoja na Taifa kwa ujumla.


More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi