December 31, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Machifu wampongeza Rais Samia kwa kuenzi utamaduni

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

VIONGOZI wa Kimila kutoka mikoa mbalimbali nchini, wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha Tamasha la Utamaduni la Kitaifa pamoja na kuongeza thamani ya viongozi wa mila iliyoonekana kushuka kwa miaka mingi.

Wamesema hatua hiyo ya kuthamini, kufufua misingi na kuenzi tamaduni zilizokuwa zimeanza kuwekwa kando itasaidia kwa kiwango kikubwa kulinda maadili na tamaduni za Kitanzania.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mkoani Ruvuma linakofanyika kongamano hilo la tatu la utamaduni la kitaifa, viongozi hao wa kimila wamesema kwa miaka mingi mila na tamaduni za Kitanzania zilionekana kutokuthaminiwa lakini Rais Samia ametambua umuhimu wake na kufufua.

“Tunamshukuru Chifu Hangaya (Rais Samia), yeye kama kiongozi namba moja wa Machifu wote Tanzania, ameona umuhimu wa kuenzi mila na tamaduni zetu ambazo zilikuwa zimeachwa kupewa kipaumbele sana, kwa kifupi ni kwamba amezifufua na kuupa thamani kubwa utamaduni wa Mtanzania, na kwa kuwa yeye ndiye msimamizi mkuu, tunaamini maadili ya nchi yetu yatalindwa zaidi,”amesema Chifu Nyamironda, ambaye ni Katibu Mtendaji wa Umoja wa Machifu Tanzania.

“Leo hii viongozi wa kimila wanakaa pamoja, wanajadili mstakabali wa taifa lao, hili  ni jambo jema sana na tunaamini hili litazidi kulinda pia utulivu na amani kwenye nchi yetu kwa sababu viongozi wa kimila wana nafasi na nguvu kubwa kutoka kwenye jamii zao wanazoziongoza.”

Belinje Yasini, Mwenyekiti wa Machifu mkoa wa Dodoma, amesema kati ya tunu ya kujivunia ni kuwa Mtanzania na kwamba, umoja na mshikamano uliopo mpaka sasa, unapaswa kulindwa zaidi.

“Amani, umoja na mshikamano tulionao ni vya kulindwa sana kwa sababu kuna baadhi ya mataifa yanatamani kuwa kama sisi lakini hayawezi, sisi tunakaa pamoja, tunazungumza lugha moja, ni wakarimu, wenye upendo na utulivu licha ya kuwa tuna makabila mengi, lakini bado tunadumisha na kulinda umoja wetu tofauti na ilivyo kwa mataifa mengine,”anasema Chifu Yasini.

“Yaani tungekuwa na ukabila, tukabaguana, tukatengana, tungeenda kuishi wapi, lakini taifa teule, lililobarikiwa kuliko mataifa yote, tunamshukuru Mungu bado tumezidi kuwa na mshikamano na amani, ni vema tukaendelea kulinda tunu hii ambayo tumepewa na Mwenyezi Mungu.”

Chifu Yasini anasema kitendo cha Rais Samia kutambua mchango wa viongozi hao wa dini ni jambo jema na anapaswa kupongezwa na kuungwa mkono kutimiza azma yake ya kuhakikisha Tanzania inaendelea kulinda tamaduni na maadili yake.

“Tumekuwa na viongozi wengi waliopita katika nafasi hiyo ya Rais, lakini hawakuzipa nguvu kubwa tamaduni zetu kama ilvyo kwa Rais Samia, kwa hiyo tunamsifu katika hili, tumuunge mkono ili kurejesha tamaduni zetu na kupambana na tamaduni potofu zisizo zetu ambazo zimeanza kuchangia mmonyoko wa maadili kwenye taifa letu,”anasema Chifu Yasini.

 “Tushirikiane na Rais Samia kupambana na vitendo vinavyochangia mmomonyoko wa maadili katika taifa letu, yeye ameonyesha njia na sisi tufuate.Tunapoona leo kuna unyanyasi, ukatili wa kijinsia na vitendo vingine vinavyotokea sasa, kazi ya kupambana navyo siyo ya serikali pekee, ni ya sisi sote jamii.”

Anasema viongozi wa mila wana mchango wa kipekee katika kujenga taifa lenye mshikamano, amani, utulivu na kuchangia katika maendeleo endelevu yanayozingatia urithi wa kitamaduni na maadili ya kitaifa.

Chifu Yasini amesema viongozi hao wa kimila wamekuwa hawashirikishwi kwenye mambo mengi kwa kutokuthamini umuhimu wao.

“Unakuta mtu anatoka mbali huko anakuja anakusanya watu kupiga kampeni lakini kiongozi wa mila wa eneo husika hashirikishwi na ndio maana wakati mwingine baadae huwa mambo yanakuja kutugharimu au kuharibika, kwa hiyo thamani aliyoionyesha Rais Samia kwa sasa kwa viongozi hawa liwe funzo kwa wengine na naamini tutafika mbali,”anasema Chifu Ismail Hassan kutoka Nachingwea mkoani Lindi.