Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOnline
MBUNGE wa Jimbo la Ilemela, Dkt Angeline Mabula, amekabidhi gari la wagonjwa kwa hospitali ya Wilaya ya Ilemela na vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na kadi 1,500 za kliniki kwa watoto wachanga, kadi 1,500 za wanawake wajawazito na vitanda 23 kutoka taasisi ya urafiki kati ya nchi ya Tanzania na China .
Akikabidhi vifaa hivyo katika hafla fupi iliyofanyika ndani ya viwanja vya kituo cha afya Buzuruga, Dkt Angeline Mabula, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hasan kwa kuipa kipaumbele sekta ya afya pamoja na juhudi zake za kutoa fedha zinazotumika kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya sekta hiyo huku akiwataka wananchi wa jimbo hili kumpongeza na kumuunga mkono kwa kumpa kura nyingi za ndio kitakapofika kipindi cha uchaguzi mkuu mwaka 2025.
“Pamoja na bajeti ya Serikali bado tunahitaji wadau wengine watushike mkono kwa ajili ya kusonga mbele, Lengo ni kupunguza umbali wa mwananchi kupata huduma, Tunahitaji kuona huduma za afya zinaimarika,” amesema.
Aidha Dkt Mabula ameishukuru Taasisi ya Urafiki wa nchi ya Tanzania na China kwa msaada wa vitanda vitakavyotumika kwenye vituo vya kutolea huduma katika wilaya hiyo pamoja kuwaomba kuendelea kushirikiana katika kumaliza kero na changamoto zinazokabili sekta ya afya ndani ya Jimbo lake.
Amewataka watumishi wa afya kuvitunza vifaa vilivyotolewa pamoja na kuwakaribisha wadau wengine wa maendeleo kwa ajili ya kushirikiana nae kuwaletea wananchi wake maendeleo.
Kwa upande wake mwakilishi wa taasisi isiyo ya kiserikali ya urafiki wa nchi ya Tanzania na China, Joseph Kahama, licha ya kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri inayofanya katika kuboresha sekta ya afya, amempongeza Mbunge Mabula kwa kujituma kwake katika kutafuta ufumbuzi wa kero zinazokabili wananchi wake kwa wadau huku akimuahidi nafasi za vijana kutoka ndani ya Jimbo lake kwenda kusoma nchini China kozi za muda mrefu na muda mfupi kwa ufadhili wa Serikali ya watu wa China.
Naye Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Buzuruga, William Ntinginya mbali na kumshukuru Mbunge Dkt. Mabula kwa vifaa vilivyokabidhiwa katika kituo chake, ameahidi kuvitunza vifaa hivyo sanjari na kuongeza kuwa kituo chake kinakabiliwa na changamoto ya kuhudumia wananchi wengi kuliko uwezo wake hivyo kuomba kuongezwa kwa bajeti ya kituo hicho ili kiweze kuwa na ufanisi katika kutoa huduma.
Manusura Sadick ni diwani wa kata ya Buzuruga, Yeye alishukuru Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mabula kwa kukabidhi vifaa hivyo huku akisema kuwa upo mpango wa kujenga jengo la mionzi (X-ray) hivyo kuomba ushirikiano wa viongozi na wananchi katika shughuli za maendeleo.
Beatrice Simon ni mwananchi wa Kata ya Buzuruga ambae alishukuru kwa gari la wagonjwa kwani litasaidia upatikanaji wa huduma za haraka pindi wagonjwa wanapozidiwa hasa wanawake wajawazito na watoto
More Stories
Madaktari bingwa wa Samia watua Rukwa
Utashi wa Rais Samia na matokeo ya kujivunia vita dawa za kulevya nchini
Uwekezaji wa Rais Samia sekta ya afya waendelea kuwa lulu Afrika