December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mabula aanika utekelezaji ilani ya uchaguzi Nyamagana

Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza


MBUNGE wa Jimbo la Nyamagana, Stanslaus Mabula,amewasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM)katika kipindi cha miaka minne (2020-2024) akijivumia utekelezaji kwa kiwango.

Mabula aliwasilisha taarifa hiyo Desemba 22,2024,katika Mkutano Mkuu wa CCM Jimbo la Nyamagana,uliohudhuriwa na wajumbe 666 kati ya 750 ambapo mgeni ramsi alikuwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda.

“Kipekee namshukuru Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha za maendeleo katika Jimbo la Nyamagana ili kuboresho sekta zinazowagusa wananchi moja kwa moja,kati ya tirioni 5.6 zilizoletwa mkoani Mwanza, Nyamagana tulipata zaidi ya bilioni 400,”amesema Mabula.

Amesema,katika kipindi cha miaka minne miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta za afya,elimu,maji na barabara,imetekelezwa kwa kiwango ikiwemo vituo vya afya na zahanati 97 zimejengwa vikiwemo vya sekta binafsi.

Pia amesema sekta ya elimu hadi kufikia Novemba 30,mwaka huu,zaidi ya bilioni 29.6 za elimu bila malipo zilipokelewa,shule za msingi nane zenye thamani ya zaidi ya bilioni 2.7 zimejengwa na sekondari nne kwa bilioni 2.03.

Mabula amesema,Jimbo la Nyamagama lilipata bilioni 1.8 kati ya bilioni 3 za miradi ya BBT,zilizoelekezwa katika sekta ya uvuvi ambapo vijana walinufaika kwa kufanya ufugaji wa samaki kwa vizimba huku Jiji likitenga milioni 500 za kuwaongezea nguvu.

Amesema kwa miaka mitatu na nusu,Jiji la Mwanza (Nyamagana),suala la maji kilikuwa kilio kikubwa na miundombinu ya barabara,hivyo serikali imejenga chanzo kipya cha maji Butimba ili kuwaondolea wananchi kadhia hiyo.

“Mradi wa maji Butimba umekuwa mkombozi lakini tumeongezwa bilioni 49 za kujenga matenki ya kuhifadhi maji huko Sahwa,Mkolani na Fumagila,ifikapo Januari mwakani,ndoto ya Nyamagana kuondokana na adha ya maji tutakuwa tumepiga hatua,”ameeleza Mabula.

Kuhusu miundombinu Mbunge huyo wa Nyamagana,amesema,kuna km 1,020 za barabara zinazopitika si zaidi ya asilimia 35,lakini katika uongozi wa Rais Dk.Samia,TARURA imepata bilioni 20 za kusaidia ujenzi wa barabara za pembezoni kwa kutumia zege na mawe yakiwemo madaraja madogo madogo.

“Barabara Kuu ya Kenyatta-Shinyanga,itajengwa kwa njia nne kuanzia Igogo hadi Usagara baada ya zabuni kutangazwa.Madaraja ya Mabatini na Mkuyuni yamekuwa yakisababisha maafa,sh.bilioni 11 zimepatikana, sh.bilioni 5zitaumika kujenga daraja la Mkuyuni na Mabataini sh.bilioni 6,”amefafanua Mabula.

Aidha,ameeleza kuwa bilioni 10 zilishatengwa za ujenzi wa barabara ya Mkuyuni,Tambukareli,Mahina hadi Mwatex kwa kiwango cha lami,lakini bado mkandarasi hajapatikana.