November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Maboresho yanayofanywa na Rais Samia kwa Mahakama yavutia mataifa mengi

Na Mwabdishi Wetu, Dodoma

MABORESHO makubwa yanayoendelea kufanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Uongozi wa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan yanaonekana kuwa kivutio kwa nchi mbalimbali duniani kuja kujifunza namna ambavyo Mahakama inaendesha shughuli zake sambamba na kufahamu mbinu zinazotumika katika kuboresha huduma ya utoaji haki kwa wananchi.

Mahakama ya Tanzania mnamo Agosti 17, 2024 ilipokea Ujumbe kutoka Mahakama ya Malawi uliofika kwa lengo la kujifunza namna ambavyo Mahakama nchini inavyofanya kazi na ilivyofanikiwa kuboresha huduma ya utoaji haki kwa wananchi.

Kadhalika hivi karibuni Jaji Mkuu wa Somalia alitembelea pia jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha, kadhalika Jaji wa Mahakama ya Juu ya Korea anatarajia kutembelea Mahakama Septemba. Nao Mahkama Kuu ya Zanzibar imepanga kutembelea Mahakama nchini kwa lengo la kujifunza.

Akizungumza juzi katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Vizano jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi cha kuanza kwa Mafunzo ya kujengeana na kubadilishana uzoefu kilichojumuisha ujumbe huo kutoka Mahakama ya Malawi na wenyeji wao kutoka Mahakama ya Tanzania, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Eva Kiaki Nkya ameukaribisha ujumbe huo na kusema kuwa wapo tayari kutoa uzoefu wa safari ya maboresho.

“Ninawakaribisha kwa moyo mkunjufu wajumbe kutoka Mahakama ya Malawi, wakiongozwa na Edith Chikagwa, Mtendaji Mkuu kwa uamuzi wenu wa kuja kujifunza Mahakama ya Tanzania, hii ni heshima kubwa kwetu, tunathamini sana fursa hii ya kubadilishana uzoefu muhimu unaolenga kuimarisha utoaji wa haki kwa watu wetu na yataendeleza malengo yetu ya pamoja na kuimarisha uhusiano kati ya mataifa yetu mawili,” alisema Nkya.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Msajili Mkuu aliueleza ujumbe huo kuwa, safari ya maboresho ya Mahakama yalikuja kufuatia Mabadiliko makubwa yaliyokuja mwaka 2011 kwa kupitishwa kwa Sheria ya Utawala wa Mahakama, ambayo ilianzisha Ofisi za Mtendaji Mkuu na Msajili Mkuu wa Mahakama, pamoja na Mfuko wa Mahakama.

“Mabadiliko haya yalikuwa mwanzo wa mageuzi ya Mahakama na kusababisha Mpango thabiti wa uboreshaji wa huduma ambao unasisitiza uboreshaji wa upatikanaji wa haki, kuimarisha ufanisi wa Mahakama, kuhakikisha uwazi na kukuza ushiriki wa wananchi,” alisema Nkya.

Aliongeza kwamba, Mahakama ya Tanzania imefanya juhudi kubwa kuboresha miundombinu ya Mahakama, kurahisisha michakato ya usimamizi wa mashauri na kuimarisha teknolojia ili kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Alieleza kuwa, safari ya kuelekea mageuzi haijawa na changamoto zake kwakuwa, Ripoti za kihistoria, kama vile ya Tume ya Msekwa ya mwaka 1977 na Ripoti ya Bomani ya mwaka 1986, zilibainisha masuala muhimu yanayokwamisha ufanisi wa Mahakama ambapo Ripoti hizo zilitaka mageuzi ya kimuundo, ufadhili wa kutosha na kuanzishwa kwa wasimamizi waliofunzwa ili kuwaondoa Maafisa wa Mahakama katika kazi zisizo za Mahakama.

“Ili kuhakikisha ufanisi wa ajenda yetu ya mageuzi, tulifanya uchambuzi wa kina wa hali ili kubainisha maeneo muhimu yanayohitaji kuzingatiwa. Uchambuzi huu ulifichua changamoto kadhaa kubwa ndani ya Mahakama, hasa kuhusu miundombinu ya Mahakama, mifumo ya usimamizi wa kesi na uwekaji kumbukumbu,” alisema Msajili Mkuu.

Sambamba na hilo, Nkya alisema kuwa, ili kupima hisia za umma kuhusu utendaji kazi wa Mahakama, Utafiti wa Kuridhika kwa Watumiaji wa Mahakama uliofanywa na REPOA mwaka 2015 ulionyesha kuwa ni asilimia 61 tu ya watumiaji walioridhika na huduma za Mahakama na kwamba uchunguzi mwingine uliofanywa na Taasisi hiyo mwaka 2019 ulionesha uboreshaji mkubwa ambapo kiwango cha kuridhika kilipanda hadi asilimia 78 na mwaka 2023 kiwango cha kuridhika kilipanda hadi asilimia 88.

Kadhalika, aliongeza kuwa, Mahakama iliandaa Mpango Mkakati wake ambao nao unalenga kuimarisha mfumo wa utawala, kuboresha kasi ya upatikanaji wa huduma za Mahakama, kujenga imani katika mfumo wa mahakama kupitia uwazi na ushirikiano wa dhati na wadau.

Msajili Mkuu ametaja maeneo ya maboresho kuwa ni pamoja na Matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika shughuli za Mahakama ambayo yamerahisisha michakato yote, kuanzia kuwasilisha faili hadi uamuzi, uboreshaji wa miundombinu ya majengo ya Mahakama ikiwemo ujengo wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki (IJCs) na Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia, utoaji huduma katika Mahakama Zinazotembea, maboresho ya kanuni za Mahakama na mengine.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Malawi, Bi. Edith Chikagwa ameishukuru Mahakama ya Tanzania kwa kukubali ombi la Mahakama hiyo la kuja kujifunza kuhusu utendaji kazi na maboresho mbalimbali.

“Tunashukuru kwa kukubali ombi letu ambalo litatuwezesha kujifunza yote mazuri kutoka Mahakama ya Tanzania na kuyapeleka nchini kwetu lengo likiwa ni kuboresha huduma za haki, kwa hiyo tumekuja tuko tayari kujifunza,” amesema Bi. Chikagwa.

Ujumbe huo ambao umehusisha Maafisa mbalimbali kutoka Mahakama ya Malawi uko nchini kwa muda wa siku sita watapata fursa ya kupatiwa mada mbalimbali ikiwemo Mfumo wa Utendaji kazi wa Mahakama ya Tanzania, Matumizi ya TEHAMA na nyingine.