January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Maboresho usalama viwanda vya chuma Pwani yanaridhisha

Na Bakari Lulela, TimesMajira Online, Pwani

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Bunge,Uratibu, Kazi,Vijana na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama ameeleza kuridhishwa na maboresho ya miundo mbinu ya usalama na afya katika viwanda vya chuma mkoani Pwani.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Bunge,Uratibu, Kazi,Vijana na Wenye Ulemavu ), Jenista Mhagama( watatu kushoto) akiwa na mkuu wa wilaya ya Mkuranga Hadija Nasri Ally (wanne kushoto), Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA Khadija Mwenda (watano kushoto)pamoja na viongozi na wafanyakazi wa kiwanda cha Fujian Hexiangwang wakati waziri huyo alipofanya ziara katika kiwanda hicho ili kufuatilia utekelezaji wa maagizo ya kuboresha mazingira ya kazi yaliyotolewa na OSHA hivi karibuni.

Ametoa kauli hiyo mara baada ya kuhitimisha ziara yake katika viwanda vya nondo vya Fujian Hexiangwang na Lodhia Group of Companies vilivyopo wilaya ya Mkuranga ambapo pamoja na hatua iliyofikiwa amevitaka viwanda hivyo kufanya maboresho zaidi.

“Nimefarijika sana kuona yale maboresho ambayo wataalamu wetu wa OSHA waliyoyatoa ili kuboresha hali ya afya na usalama kwa wafanyakazi yametelezwa kwa zaidi ya asilimia 70. Hata hivyo bado kuna mambo ambayo tunawataka waendelee kuyaboresha ikiwemo kuweka mtambo wa kukusanya moshi ili usiharubu mazingira pamoja na afya za wafanyakazi,” amesema Waziri Mhagama na kuongeza:

“Kitu kikubwa kilichofurahisha katika kiwanda hiki cha Lodhia Group of Companies ni jinsi teknolojia wanayotumia katika uzalishaji inavyosaidia katika kukuza uchumi wa nchi. Kiwanda hiki sasa kinazalisha nondo adimu zenye ukubwa wa milimeta 40 ambazo zinauzwa hata nje ya nchi yetu.

“Hata hivyo tumebaini kuwepo kwa mapungufu kadhaa ya kiusalama na afya ikiwemo kutokuwepo kwa mashine za kubebea vyuma chakavu na kuvipeleka katika majiko ya kuyeyushia vyuma hivyo tumewashauri nao wauweke,”amesema.

Katika ziara hiyo Waziri aliambatana na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pakazi (OSHA), Khadija Mwenda, ambaye amesema ziara hiyo ililenga kufuatilia utekelezaji wa maagizo mbalimbali ambayo Taasisi yake imekuwa ikiyatoa katika viwanda hivyo.

“Katika usimamizi wa sheria ya afya na usalama mahali pakazi pamoja na kufanya ukaguzi wa kawaida katika maeneo haya kila mwaka pia huwa tunafanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa maelekezo ambayo yanatolewa na wakaguzi wetu. Hivyo leo pia tumekuja kwa ajili ya kufuatilia maagizo ambayo tuliyatoa hivi karibuni tulipokuwa tunafanya uchunguzi wa ajali zilizokuwa zimetokea katika baadhi ya viwanda vya chuma,” amesema Mtendaji Mkuu wa OSHA.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kiwanda cha Lodhia Group of Companies Salesh Pandit pamoja na wafanyakazi wa viwanda vilivyotembelewa wamemshukuru waziri na watendaji wa serikali kwa kufanya ziara na kutoa ushauri juu ya masuala mbalimbali yenye kuleta ustawi katika uwekezaji na haki za wafanyakazi.

“Kiukweli tulikuw na changamoto nyingi sana za kiusalama na afya lakini niwapongeze OSHA ambao baada ya kufanya ukaguzi waliopokuwa wakichungiza ajali iliyotokea hapa walishauri maboresho mengi sana muhimu ikiwemo mtumizi ya mashine maalumu za kupakia vyuma chakavu katika majiko ya kuyeyushia ambapo hapo awali kazi hiyo hatarishi tulikuwa tukiifanya kwa mikono yetu,” alisema Machaga Silvan ambaye ni mfanyakazi wa kiwanda cha Fujian Hexiangwang.

Mwezi mei mwaka huu zilirepotiwa ajali kadhaa katika baadhi ya viwanda vya chuma vya Dar es Salaam na Pwani ambazo zilipelekea kufanyika uchunguzi wa kina katika mifumo ya usalama na afya katika viwanda vya chuma. Kutokana na uchunguzi huo, wataalamu kutoka OSHA walishauri maboresho mbalimbali katika mchakato mzima wa uzalishaji ikiwemo kutumia mashine maalumu kupakia vyuma chakavu kwenye majiko ua kuyeyushia malighafu husika.