December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mabilioni kujenga barabara za Ilemela

Judith Ferdinand,Timesmajira Online,Mwanza

Zaidi ya bilioni 23.4 zitatumika katika mradi wa ujenzi wa barabara ya kilomita 12.8 kwa kiwango cha lami wilayani Ilemela mkoani Mwanza ambapo kata tatu za Buswelu,Nyamh’ongolo na Nyakato zitanufaika na mradi huo.

Huku wananchi wa Kata ya Buswelu wameeleza kuwa endapo mradi huo utatekelezwa na kukamilika kwa wakati utawasaidia kuwaondolea adha waliokuwa wanaipata kwa muda mrefu tangu Nchi kupata uhuru ikiwemo usafiri wakati wa kuwapeleka wajawazito kujifungua.

Katibu Tawala Wilaya ya Ilemela Mariam Msengi (wa tatu kulia) akiwakabidhi eneo la mradi Mhandisi Mshauri kutoka NMETA Mhandisi Heri Sanga(wa pili kushoto) na Mwakilishi wa Nyanza Road Works Limited wa kwanza kushoto

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi eneo la mradi (site) kwa Mkandarasi utekelezaji wa mradi wa uboreshaji wa miundombinu ya Miji ya Tanzania(TACTIC) kwa ufadhili wa Benki ya Dunia,iliofanyika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Oktoba 23,2023 , Mratibu wa mradi huo wa halmashauri hiyo Juma King’ola ,amesema mradi huo utahusisha barabara mbili.

King’ola ameeleza kuwa mradi huo unahusu ujenzi wa barabara kwa kiwango cha tabaka la lami ngumu yenye jumla la kilomita 12.8 ambazo ni barabara ya Buswelu-Nyamadoke-Nyamh’ongolo yenye Kilomita 9.5 na upana wa mita 20 na Buswelu-Busenga- Coca-cola kilomita 3.3.

“Mkandarasi anayetekeleza mradi huo ni Nyanza Roads Works Limited kwa muda wa miezi 15 huku Mhandisi Msahuri wa mradi huo akiwa ni Nimeta Consults Limited na leo Oktoba 23,mwaka huu tumewakabidhi rasmi maeneo ya kazi ili kukamilisha maandalizi na kuanza utekelezaji,”ameeleza King’ola.

Mhandisi Mkadiriaji Majenzi,Msimamizi wa Mkataba kutoka Nyanza Road Works Limited Juma Maro,ameeleza kuwa miradi yote miwili itakamilika Janauari 22,2025.

Mhandisi Maro ameeleza kuwa mradi wa barabara ya Buswelu-Busenga-Coca-cola utaanza Novemba 20,2023 hadi Machi 30,2024 na Buswelu-Nyamadoke-Nyamh’ongolo itaanza Februari 23,2024 hadi Desemba 9,2024.

“Baada ya kukamilisha ujenzi itabaki shughuli ndogo ndogo ya kumalizia kufunga taa hivyo kazi yote itakamilika mwaka 2025,tutatekeleza mradi kwa kiwango na utakamilika kwa wakati kwa mujibu wa mkataba,”ameeleza Mhandisi Maro.

Mhandisi Mshauri wa mradi huo Heri Sanga kutoka Nimeta ameeleza kuwa Mkandarasi huyo atatekeleza mradi huo kwa muda wa miezi 27 kwa maana ujenzi ni miezi 15 huku miezi 12 ya uangalizi.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilemela Mariam Msengi aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Ilemela,amemtaka mkandarasi huyo atakapo anza utekelezaji hakikishe unakamilika kwa wakati na kiwango ili kuondoa adha iliopo kwa wananchi.

Muonekano wa barabara ya Buswelu-Nyamadoke-Nyam’hongolo ambayo itajengwa kwa kiwango cha lami kwa urefu wa kilomita 9.5 kupitia mradi wa TACTIC huku kulia ni muonekano wa eneo ambalo mwananchi amebomoa kwa ajili ya kupisha ujenzi huo

Naye mmoja wa wananchi wa Buswelu John Elias,ameeleza kuwa barabara ya Buswelu-Busenga-Coca-cola ni kiunganisho kikubwa kwa wakazi wa maeneo hayo changamoto iliopo ni ubovu ambao wakati wa masika haipitiki kabisa na kusababisha uchumi wao kushuka na kushindwa kupata huduma kwa urahisi.

“Endapo barabara hii ikijengwa kwa kiwango cha lami itakuwa ni kiunganishi muhimu sana kwa wanachi wa Buswelu,Igoma na viunga vyake na kuchochea uchumi wa maeneo hayo,”amesema John.

Stella Alyoce ameeleza kuwa ubovu wa barabara hiyo kunawapa wakati mgumu wananchi wa eneo hilo hasa wajawazito akitolea mfano binti yake kipindi cha nyuma alivyotaka kujifungua ilikuwa ni shida kwa sababu gari alifiki huko kwa ndani.

Hivyo walilazimika kutumia usafiri wa bodaboda ambao ni hatari kwa mjamzito kwani anaweza kujifungulia njiani kutokana na kurushwa kurushwa jambo ambalo anaeleza kuwa ni hatari kwa maisha ya mama na mtoto.

“Tunashukuru kwa serikali kuamua kujenga barabara hizi kwani tunaangaika ukiwa na mizigo kuleta dukani tunapata shida hasa wakati wa mvua ndanindani huku ni mabonde mvua ikinyesha kunakuwa na utelezi na michanga kujaa,” ameeleza Stella.

Muonekano wa barabara ya Buswelu-Busenga-Coca-cola ambayo itajengwa kwa kiwango cha lami kwa urefu wa kilomita 3.3 kupitia mradi wa Tanzania(TACTIC)

Naye Diwani wa Kata ya Buswelu Sarah Ng’hwani amewashauri wakandarasi wakati wakitekeleza shughuli zao wawashirikishe madiwani na wenyeviti wa mitaa wakati wa kuainisha njia za mchepuko.