December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mabadiliko ya tabianchi yanavyohatarisha wananchi wa Ngelenge

Na Penina Malundo,timesmajira,Online

WAKATI mataifa mbalimbali duniani yakiendelea kutafuta ufumbuzi wa kudumu ili kuyakabili mabadiliko ya tabia nchi,madhara ya mabadiliko hayo yameanza kuwa mwiba kwa wanawake ambao kwa sasa wanakumbana na vipigo na tuhuma mbalimbali kutoka kwa waume zao.

Kwa mujibu wa Jopo la Kimataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (IPCC) ambalo lilibuniwa na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) kwenye ripoti yake ya Tano ya Tathmini inaeleza kuwa, mabadiliko ya tabianchi yapo na shughuli za binadamu, hasa kuachiliwa kwa gesi chafuzi kutokana na kuchoma fueli ya visukuku (makaa ya mawe, mafuta, gesi) ndicho chanzo kikuu.

WANASEMAJE

Bernadina Nchimbi ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Ngelenge kilichopo Kata ya Ruhuhu Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe amesema, kijiji chao kimekuwa na changamoto kubwa sana ya maji kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Amesema, mabadiliko hayo ya tabianchi yamewasababishia changamoto mbalimbali ikiwemo ya vipigo kwa waume zao kutokana na ukosefu wa maji, kwani ujikuta wanatumia muda mrefu kwenda kuyatafuta maji, hivyo waume zao kuwatuhumu kuwa, wanatumia fursa hiyo kwenda kutenda vitendo vya uzinzi.

Nchimbi amesema, sababu ya kufuata maji umbali mrefu umewafanya baadhi ya wanawake wa kijiji hicho kupigwa mara kwa mara na waume zao kutokana na kuchelewa kurudi nyumbani.

“Wiki iliyopita nilienda kuchota maji Mtoni kuna umbali mrefu sasa nilipokuwa narudi nyumbani nilimkuta Bwana angu (mumewe) amerudi yupo nyumbani ile nashusha ndoo kichwani tu akaanza kunipiga kisa sijampikia chakula,akaanza kunihoji wapi nilipochelewa na mimi nikamwambia nilikuwa nachota maji,”amesimulia

Amesema, ni mara ya tatu tayari amempiga kwa kisa cha kuchelewa kwenye maji na kushindwa kumpikia chakula mapema.

“Nilienda kutoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Kitongoji juu ya kupigwa na mume wangu kisa maji,ila hadi sasa hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa dhidi yake,”amesema.

Aidha,anaiomba serikali iwasaidie kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji katika kijiji chao kwani wamekuwa wanapata changamoto kubwa ambazo wao wanawake ndio wahanga wakubwa.

“Tunachota maji katika mazingira magumu sana sana,mto unamamba wengi hatuwezi kuchota maji kwa pamoja tunachota maji kwa awamu awamu na eneo tunalochota maji hatujui kama linamamba hivyo unashtukia kitu kinakurukia tu na kuchukua ndoo,”anasema na kuongeza

“Tupo katika hatari kubwa sana kuhatarisha maisha yetu,huku tunapokea vipigo kwa wanaume zetu tukichelewa kurudi nyumbani huku tunaliwa na Mamba Mtoni,”amesema.

Amesema, mwaka jana kuna jirani yao alitoka alfajiri kama kawaida yake kwenda kuchota maji kufika huko Mamba akamla hivyo imekuwa ni hatari sana kwao ila hawana namna ya upatikanaji wa maji ni lazima waende wakachote maji katika Mto kwaajili ya matumizi yao.

Sophia Komba (14) ni Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Manda kata ya Manda Mkoani Njombe amesema yeye kama mwanafunzi amekuwa akipata changamoto kubwa wa kusoma huku kutafuta maji.

Amesema kawaida uamka alfajiri ya saa 11 kisha uenda mtoni kuchota maji na baadae kujiandaa kwenda shuleni ambapo masomo uanza saa mbili asubuhi.

“Tumekuwa tukipata changamoto kubwa hata kwetu wanafunzi ni lazima tuamke asubuhi tukachote maji kisha twende shuleni,hapo ukichelewa namba shuleni unachapwa huku nyumbani napo unapigwa sababu ya maji,”anasema na kuongeza,

“Jana tu mama alinipiga kisa kuchelewa kurudi nyumbani,na kosa sio langu nilikuta mtoni kuna watu wengi ndipo niliporudi nyumbani akaanza kunipiga,”anasema.

Wanakijiji wa Kijiji cha Ngelenge kilichopo Kata ya Ruhuhu Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe wakiwa wanachota maji katika mto wa ruhuhu.

Kwa Upande wake Esau Lunga Mkazi wa Kijiji hicho amesema licha ya maji ya mto huo yanawasaidia ila ni machafu kutokana na baadhi ya migodi ya madini kutumia maji hayo katika kuosha madini yao.

Amesema licha ya kuwa na tabu ya upatikanaji wa maji katika eneo lao lakini Serikali ingewasaidia hata kuwatuma watafiti kujua maji hayo yanaathari gani kwao na yanamadhara gani ili waweze kuchukua hatua kabla ya matatizo kuyakumba.

“Wakinamama wamekuwa wakidamka saa 11 alfajiri kwenda kuhangaika na maji,visima vimekauka maji hakuna maji kabisa hii ni namna mabadiliko ya tabianchi yalivyotusababishia hali hii tunaomba tusaidiwe,”anasisitiza

Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ngelenge,Christandus Komba anasema tatizo la maji ni janga kubwa katika Kijiji chake ambacho kinakaya ya takribani 3500 katika vitongoji vinne ambapo lilianza July ,2020 watu kuanza kuangaika na maji kwenda kuchota katika Mto ruhuhu kijiji cha Ngelenge wilayani Ludewa mkoani Njombe.

Anasema tatizo la maji lilianza baada ya ongezeko la wakazi wa Kijiji chake hivyo kupelekea kisima ambacho kilikuwa kikiwahudumia kaya 1500 ya watu kuzidiwa.

“Tumekuwa na Changamoto kubwa Sana hasa kipindi hiki cha mabadiliko ya tabianchi,licha ya jitihada mbalimbali kuchukua kunusuru wananchi wangu ikiwemo kukutana na Diwani na kuzungumza nae juu ya tatizo hili ambapo hali inazidi kuwa mbaya zaidi,”anasema na kuongeza

“Tumekubaliana na diwani kuandika mutasari ambao tutaupeleka halmashauri kuona ni namna gani watakavyotusaidia,ila hali ni mbaya wakinamama wanaliwa na Mamba mtoni tayari watu wawili wameliwa mmoja mwaka juzi na mwingine mwaka jana,”amesema

Amesema mbali na hiyo maji yenyewe ya mtoni nayo sio salama ila kwa kuwa watu hawana maji na visima havina maji inapelekea kuchota hayo hayo na kutumia.

“Hali za ndoa nazo ni shida wanaume wamekuwa wakiwapiga wake zao kisa kuchelewa kurudi nyumbani,nimekuwa nasuluhisha ugomvi kila mara na kuelekezana juu ya changamoto tuliyonayo hivyo wavumiliane,”amesema

MTAFITI WA MAZINGIRA

Mtafiti , Mtaalamu na Mshauri wa masuala ya Jinsia na Mabadilio ya Tabianchia ambapo awali alikuwa Ofisa wa Baraza la Uhifadhi wa Mazingira (NEMC),Dkt Lucy Ssendi amesema kuna utafiti aliofanya kupitia jukwaa ambalo linafahamika kama Climate Change and Development Learning Platform kwa ufadhili wa Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania,ambao unaonyesha kuwa uhusiano kati ya madhara ya mabadiliko ya tabianchi, hali ya hewa na ukosefu wa usawa wa kijinsia unavyoathiri ufanisi wa utoaji huduma mbalimbali kwa wanawake na wasichana.

Amesema uchanganuzi wa athari za mabadiliko ya tabianchi kwa siku zijazo hadi mwaka 2040 kwa kilimo kinachotegemea mvua unaonesha mwelekeo endelevu wa uwezekano wa kuwepo ongezeko la joto.

Amesema taarifa za uchunguzi na utabiri wa hali ya hewa unaonesha kwamba madhara yanayohusiana na hali ya hewa kwa kaya zinazotegemea kilimo na kaya nyingine maskini yataongezeka, kama ilivyo kwa kuenea kwa magonjwa ya mlipuko kutokana na mabadiliko ya tabianchi .

“Makadirio ya mabadiliko ya tabianchi yanaonesha kwamba mabadiliko ya misimu na majira kila mwaka yataongezeka kwani masuala ya kijamii na kiutamaduni yanasababisha kwa kiasi kikubwa unyanyasaji wa kijinsia, ukiwemo usimamizi na udhibiti, usio sawa, wa mapato yatokanayo na shughuli za kilimo,”anasema na kuongeza

“Kuna ukosefu mkubwa wa usawa kwenye maamuzi ndani ya kaya kuhusiana na matumizi ya mapato yatatokanayo na kilimo na ufugaji,wanawake na wasichana wana kauli ndogo au hawana kauli kabisa kwenye kufanya maamuzi haya,”amesisitiza.

Amesema ubaguzi wa kijamii na kiutamaduni dhidi ya wanawake na wasichana ni kichocheo kinachowaweka karibu sana na madhara yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi.

“Uwezo mdogo wa kuhimili athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi na mikakati iliyopo inawafanya wanawake na wasichana kuwa kwenye hali ngumu zaidi,”amesema Ssendi.

Amesema ushahidi uliojitokeza unaoonesha kwamba kuna wanawake na wasichana ambao ni rahisi kuhadhirika a kwa kiwango kikubwa na mabadiliko ya tabianchi hususani katika unyanyasaji wa kijinsia ambapo unaongezeka kadri mabadiliko ya tabia nchi yanavyoongezeka.

WATAALAM WA MAZINGIRA WASEMAVYO

Sara Pima ni mmoja wa Wataalamu wa Mazingira na pia ni Mkurugenzi wa Taasisi y ya Hudefa amesema mabadiliko ya tabianchi yanachangia kwa kiasi chake ukatili wa kijinsia ambapo wanawake na wasichana ndio wanaonekana kuwa wahanga wakubwa katika hili.

Amesema ukame umekuwa ukiwaathiri wanawake wengi hususani wale wanaoishi vijijini hali ambayo inawaletea athari nyingi ikiwemo kupata vipigo kutoka kwa wanaume zao.

“Katika kupinga siku 16 za ukatili wa kijinsia tukumbuke namna ya mabadiliko ya tabianchi yanavyochangaia kwa kiasi chake katika ukatili wa kijinsia hasa katika kundi la wanawake na wasichana wengi,”amesema na kuongeza

“Mabadiliko ya tabianchi yanapotokea yanasababisha hali ya ukame ambapo upatikanaji wa maji unakuwa mgumu na kusababisha wanawake wengi hasa hasa wasichana kutembea umbali mrefu wa kutafuta maji,”amesema

Aidha amesema wakati mwingine wanapokuwa wakitafuta maji kwa umbali mrefu ukutana na changamoto mbalimbali ikiwemo kufanyiwa vitendo vya ubakwaji au kukutana na Wanyama wakali.

“Huko maeneo ya vijijini ndipo kwenye hali mbaya zaidi watu wanatafuta maji kwa umbali mrefu na wakiwa njiani wanakumbwa na changamoto mbalimbali na kuwafanya kutotimiza ndoto zao hasa kwa Watoto wa kike,” anasema

Amesema unakutwa mtu anafanyiwa kitendo cha kubakwa na hapo anaweza kupata ujauzito na ndipo inakuwa mwisho wa ndoto zake hasa kwa mabinti ambao waliokuwa shuleni.

Pima amesema lipo suala la mafuriko nalo ni miongoni mwa mambo ambayo yanachangia kwa kiasi kikubwa suala la ukatili wa kijinsia katika mabadiliko ya tabianchi.

Ameeleza asilimia kubwa ya wanawake ndio wahanga wakubwa katika hili kwani kundi kubwa la wanawake uwa ni watu wa majumbani.

Pima amesema mvua inaponyesha mara nyingi uwakuta wakiwa nyumbani hivyo mafuriko yanapotokea wanawake wanakuwa nyumbani na Watoto hivyo uwapelekea kupata shida katika harakati za kujiokoa.

“Wamama wengi ni mama wa majumbani mafuriko yanapotokea wao ndio wanakuwa wahanga wakubwa katika hili na kuwafanya waathirike kiuchumi kutokana na kupoteza vitu vyao,”amesema

Aidha amesema wakati mwingine mafuriko yanakuwa yanawachukua watu kutokana na maji kutembea kwa spidi kubwa hivyo kusababisha vifo kwao kutokana na wanawake kutokuwa na uwezo wa kujiokoa wenyewe.

“Suala hili la a mafuriko nalo ni miongoni mwa ukatili wa kijinsia ambao imekua likiathiri sana ukatili wa kijinsia kwa namna yake,”amesema na kuongeza

“Mara nyingi mafuriko yanapotokea kuna muda wanawake wengine uokolewa na kuwekwa katika kambi mbalimbali za kujihifadhi lakini katika kambi hizo kuna matukio yanayotokeaga ambayo yanakuwa ni kinyume cha utu kwao,”amesema.

Pima amesema wanawake hao ujikuta kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa baadhi ya watu wanaoishi nao katika makambi hayo kwa kuwanyanyasa kuwanyima vyakula vya msaada na kuwaradhimu kuingia katika vitendo ambavyo sio vya kiungwana.

Amesema inafikia mahali katika makambi hayo wanawake wanabakwa na wengine kulazimisha kufanya ngono na hii yote inatokana na athari au chanzo cha mabadiliko ya tabianchi.

Kwa Upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Jielimishe Kwanza, Henry Kazula amesema kuna uhusiano mkubwa sana kati ya mabadiliko ya tabianchi na vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Amesema mabadiliko hayo ya tabianchi yanaathari zake zinawakumba tofauti kati ya wanaume na wanawake ambapo wanawake ndio wanaonekana kuathirika zaidi kutokana na mabadiliko ya majukumu ya kila siku.

“Mabadiliko hayo ikihusisha upatikanaji wa maji ,kuni na pia uwezo wa kuhimili majanga pale yanapotokea inakuwa tofauti,”amesema na kuongeza

“Mabadiliko ya tabianchi yanachochea vitendo vya ukatili wa kijinsia,kutokana na majanga yanapotokea wahanga wakubwa wanakuwa wanawake na yanapotokea wanakuwa katika vitendo hatarishi zaidi hususani kuvamiwa na kubakwa,”amesema

Kazula amesema kunahitajika kuleta hamasa zaidi hususani kipindi hiki cha siku 16 za kupiga ukatili wa kijinsia kutojitikeza katika jamii jamii isiache nyuma kutozungumzia masuala ya mabadiliko ya tabianchi kwani athari zake ni kichocheo kikubwa cha vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Amesema sekta ya kilimo nayo inawaathiri zaidi wanawake kutokana na mabadiliko ya tabianchi na hii inawaathiri kwa sababu wanakosa uwezo wa kulima na kuzalisha kwa kiwango kinachotakiwa.

“Unakuta mafuriko yanapotokea au mvua ikiwa chache uzalishaji unapungua au wakati mwingine mazao yanaharibika kutokana na maji mengi au mazao yanadumaa,”amesema na kusisitiza

“Asilimia 75 ya wanawake nchini Tanzania wamejikita na shughuli za kilimo hasa waishio vijijini na wakitegemea kilimo kujikimu kwa mahitaji ya kila siku,”amesema.

KAULI YA MBUNGE WA LUDEWA

Mbunge wa Jimbo la Ludewa, Joseph Kamonga amekiri ni kweli eneo hilo linachangamoto ya maji na watu wake kuangaika na hii no kutokana na baada ya pumpu kuharibika na kuwafanya wananchi wa eneo hilo kuangaika kutafuta maji.

Amesema tayari amezungumza na Waziri wa Maji Jumaa Aweso na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo juu ya tatizo hilo na kupeleka fedha kwa ajili ya matengenezo ya Bomba hilo.

“Mwaka Jana Naibu Waziri wa Maji aliwahaidi Bilioni 1 kukarabati maji ambapo kiasi cha sh.Milioni 500 zitatolewa kwaajili ya kukamilisha miundombinu ya maji katika Shule ya Sekondari ya Manda kata ya Ruhuhu,”amesema na kuongeza

“Serikali imechimba kisima ambapo kwa sasa inatandaza Mitambo ya maji zaidi kwa kiasi cha sh.Milioni 155 katika vijiji vya Mbongo,”amesema

Aidha amesema katika kijiji cha Ngelenge Ngelenge mradi wa kisima ambapo pumpu zake zilikuwa zimekufa,aliweza kuwasiliana taarifa hiyo serikali na walihaidi kuingiza katika mpango wa bajeti 2022/2023.

“Mradi huu utakapo kamilika utaweza kuhudumia watu wapatao 1300 katika kijiji cha Ilela kata ya Ruluhu na tatizo la maji kuisha kabisa kwani mradi utakuwa Mkubwa na kufanya vijiji vya Jirani kupata maji,”amesema

TUNAPASWA KUFANYA NINI

Ili kudhibiti ongezeko la joto lisizidi nyuzijoto 1.5, tunahitaji kupunguza uzalishaji wa gesi chafu kwa asilimia 7.6 kila mwaka kuanzia mwaka huu hadi mwaka wa 2030. (EGR, 2019)

Miaka 10 iliyopita, ikiwa nchi zingechukua hatua kuhusu hii sayansi, serikali zingehitaji kupunguza uzalishaji wa gesi chafu kwa asilimia 3.3 kila mwaka.

Kila mwaka tunaposhindwa kuchukua hatua, kiwango cha ugumu na gharama ya kupunguza uzalishaji wa gesi chafu hupanda. (EGR, 2019).

Kupunguza mno uzalishaji wa methani ni muhimu ili kusaidia kupunguza ongezeko la joto duniani lisizidi nyuzijoto 1.5 au nyuzijoto 2, kwa mjibu wa IPCC.

Zaidi ya asilimia 75 ya uzalishaji wa gesi ya methani unaweza kupunguzwa na teknolojia iliyopo leo na hadi asilimia 40 bila gharama yoyote kwa mjibu wa Shirika la Kimataifa la Nishati. (Ukweli kuhusu Uzalishaji wa Methani, UNEP).

Kuhifadhi na kuboresha maeneo ya kiasili, kwenye ardhi na majini, ni muhimu ili kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa na kuwezesha kupunguza theluthi moja ya juhudi zinazohitajika katika muongo ujao. (Ukweli kuhusu Hali ya Ushughulikiaji wa Mazingira, UNEP).

Kwa kuwa zaidi ya nusu ya Pato la Taifa (GDP) duniani hutegemea mazingira kwa kiwango cha juu au kiwango fulani, kuwekeza kwenye masuluhisho yanayotokana na mazingira hakutapunguza tu ongezeko la joto ulimwenguni, lakini pia kutapelekea mapato takribani ya dola bilioni 4 kwa wafanyabiashara na kubuni nafasi mpya za ajira zaidi ya milioni 100 kila mwaka kufikia mwaka wa 2030 . (Ukweli kuhusu Hali ya Ushughulikiaji wa Mazingira, UNEP)

Kwa serikali, kuimarisha uchumi bila kuchafua mazingira baada ya COVID-19 kunaweza kupunguza uzalishaji wa gesi chafu kwa asilimia 25 kutoka kwa viwango vya mwaka wa 2030, na kuwezesha dunia kufikia lengo lake la nyuzijoto 2. (EGR, 2020).

Mataifa yalikubaliana kujitolea kisheria mjini Paris kupunguza kiwango cha joto ulimwenguni kisizidi nyuzijoto 2 zaidi ya viwango vya kabla ya viwanda lakini pia yalitoa ahadi za kitaifa za kupunguza au kuzuia uzalishaji wa gesi ya ukaa kufikia mwaka wa 2030. Huu unajulikana kama Mkataba wa Paris