December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mabadiliko ya tabianchi yanavyochangia uharibifu wa vyanzo vya maji

Na Penina Malundo,TimesMajira online

SEKTA ya maji ni miongoni mwa sekta ambazo zipo sambamba na huduma zote za kiuchumi na kijamii ambazo zimekuwa zikitegemea maji.

Kutokana na ukosekanaji wa maji huduma hizi za kiuchumi na kijamii zimekuwa zinaathiriwa moja kwa moja na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Athari hizi zimefikia hatua ya kupunguza upatikanaji wa maji safi na salama kwa kusababisha uchafuzi na uharibifu wa vyanzo vya maji vikiwemo visima na chemichemi.

Mabadiliko ya tabianchi yamechangia kwa kiasi kikubwa baadhi ya vyanzo vya maji kuingiliwa na chumvi kufuatia kuongezeka kwa kina cha bahari hasa katika maeneo ya Pwani.

Kufuatia hali hii ambayo inapelekea uhaba wa maji katika maeneo mbali mbali ya nchi, ni muhimu jamii kukumbuka kwamba athari za mabadiliko ya tabia nchi zitakuwa ni changamoto kubwa katika sekta ya maji.

Kwa upande mwingine,athari za mabadiliko ya tabia nchi zimesababisha kuathiriwa kwa upatikanaji wa maji safi na salama kwa ajili ya shughuli za usafi na huduma za afya.

Kufuatia athari hizi na changamoto zake,Serikali ya Tanzania imekwisha chukua hatua mbalimbali kupitia Sera, mipango na mikakati ikiwa ni jitihada za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Jitihada hizo ambazo zimechukuliwa na Serikali ni pamoja na uanzishwaji wa mpango wa nchi wa kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi (2015) ambao uko katika mchakato wa kukamilika, Mkakati wa nchi wa kuhimili na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi (2012) ambao uko kwenye mapitio kwasasa,pamoja na mpango mahsusi wa Taifa kuchangia jitihada za kupambana na uzalishaji wa gesi joto ambao uko katika hatua za mwisho.

Maandalizi ya mpango huu ni kukamilisha makubaliano ya ulimwengu ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi yajulikanayo kama makubaliano ya Paris (“Paris Agreements”) ya mwaka 2015 ambayo Tanzania ili ridhia utekelezaji wake.

Aidha kuna Mpango wa Taifa wa kuhimili athari za mabadiliko ya tabia nchi katika idara ya afya wa mwaka 2018-2023.

Pamoja na jitihada hizi zote za nchi,mpango wa nchi wa kuchangia jitihada za kupambana na uzalishaji wa gesi joto na kukabiliana na athari zingine za mabadiliko ya tabia nchi (National Determined Contributions-NDCs) haujahusisha mikakati ya kuhakikisha upatikanaji wa maji safi, kwa ajili ya shughuli za usafi na afya, pamoja na ukweli kwamba maeneo haya mawili yana uhusiano wa dhahiri hasa katika kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi.

Jukwaa la Mabadilko ya Tabia nchi (FORUMCC) kwa kushirikiana na Muungano wa Kikanda wa Usawa katika kukabiliana na thari za mabadiliko ya tabianchi (“Pan-African Climate Justice Alliance-PACJA) waliendesha mkutano wa wadau mbalimbali wanaoshughulikia jitihada za kuhimili na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, zikiwemo asasi za Kiraia zinazojihusisha na sekta za maji, usafi na afya (WASH).

Wadau hawa kutoka mashirika yasiyo ya Kiserikali, vikundi vya vijana na wanawake, sekta binafsi na vyombo vya habari walikutana ili kujadili na kupeana taarifa sahihi kuhusu namna bora ya kuishauri serikali kujumuisha sekta ya maji, usafi na afya (Water,Sanitation and Hygiene-WASH ) katika mpango wa nchi wa kuchangia jitihada za kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi hususani kupunguza uzalishaji wa gesi joto.

Akiwasilisha matokeo ya tathmini fupi iliyofanyika ili kubaini uwezekano wa kuchagiza uhusishwaji wa sekta za maji, usafi na afya katika mpango huo, Mtaalamu mshauri wa tathmini kutoka FORUMCC, Msololo Onditi anasema pamoja na mpango huo kuzijumuisha sekta za maji, uhifadhi wa taka na afya kama sehemu ya vipaumbele katika utekelezaji, bado mpango haujaeleza bayana ni mikakati gani itatumika kuhakikisha upatikanaji wa maji, huduma za usafi na afya zitakavyotekelezwa bila kuchagiza athari za mabadiliko ya tabia na kupunguza uzalishaji wa gesi joto.

Anasema pia mikakati hiyo inapaswa kuonesha jinsi sekta hizo zitakavyo kuwa himilivu dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Onditi anasema tathimini hiyo imebainisha kuwa mpango huo haujatoa mifano na miongozo ya teknolojia, usimamizi na uhifadhi thabiti wa taka ikiwemo majalala na usafi kwa ujumla.

Pia,mifumo ya uteketezaji na aina ya nishati itakayotumika wakati wa uteketezaji wa taka zikiwemo zile zinazozalishwa katika vituo vya huduma za afya,shughuli za uzalishaji mali na kibiashara hiajabainishwa.

“Mpango huu haujaweka wazi mikakati sahihi katika eneo hili pamoja na ukweli kwamba uteketezaji wa taka unazalisha gesi joto zikiwemo hewa ukaa katika viwango mbalimbali.

“Kadhalika, tathmini imeibaini kuwa hakuna mikakati bayana kuhusu uhifadhi wa taka za majimaji/owevu ambazo uhifadhi na uteketezaji wake una mchango mkubwa katika uzalishaji wa gesi joto na kuchagiza utokeaji wa athari za mbadiliko ya tabianchi,”anasema Onditi.

Kwa Upande wake Mtaalamu Mbobevu katika mabadiliko ya tabianchi na Maliasili,Abdallah Henku anasema mpango umejikita zaidi katika kuhakikisha uhifadhi wa vyanzo vya maji na kusahau kuwa maji yanahitaji kusambazwa ili kuwafikia watumiaji.

Anasema mpango huo hauoneshi mikakati ya usambazaji wa maji ambapo bado si suluhisho hasa katika mazingira ambayo maji yanatakiwa ili kuwezesha upatikanaji wa huduma za usafi na afya.

Naye Mwenyekiti wa bodi ya FORUMCC na Mtaalamu Mbobevu katika mabadiliko ya tabianchi na Maliasili,Euster Kibona,alisema kuwa uhusishwaji wa wananchi katika jamii hasa wakati wa maandalizi ya mipango ya kuhimili na kukabiliana na Athari za mabadiliko ya tabia nchi ni muhimu kwani kutasaidia wananchi kujifunza mambo muhimu na kupaza sauti zao pale masuala muhimu yanayogusa mustakabali wa Maisha yao yanapokosekana.

Anasema katika sekta ya afya,hatua za kuhimili na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi huwa ni dharura kiasi ambacho wahanga hawapati fursa ya kujifunza na kuchukua tahadhari.

“Kwa kuwa suala la usafi na afya linahusisha makazi ya watu,ni vema elimu ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi ikatolewa kwa maafisa wa mipango miji na wananchi kwa ujumla,”anasema na kuongeza.

“Pamoja na kutohusishwa kwa sekta ya maji,usafi na afya katika mpango huu wa nchi,bado kuna matumaini na mahala pa kuanzia kwakuwa sekta muhimu kama afya,maji na uhifadhi wa taka zimebainishwa kama maeneo muhimu ya kuchukuliwa hatua stahiki katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, “anasema Kibona.

Anasema FORUMCC na PACJA wameamua kuchukua hatua hii kwa lengo la kuleta pamoja wadau na kupaza sauti kwa waamuzi na watunga sera serikalini kutumia fursa ya kuhusisha sekta za upatikanaji wa maji, huduma za usafi na afya katika mapitio yatakayofanyika hivi karibuni ikiwa ni kuitikia wito wa jumuiya ya kimataifa kuhusisha baadhi ya shughuli za kukuza uchumi katika mipango ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.