October 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Maaskofu, wachungaji wafanya kongamano kuombea uchaguzi

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

VIONGOZI wa makanisa mbalimbali ya kiroho kutoka ndani na nje ya nchi wamekutana Wilayani Igunga Mkoani Tabora katika kongamano maalumu la siku 3 la kuombea amani na uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu nchini.

Miongoni mwa Viongozi walioshiriki Kongamano hilo ni Maaskofu na Wachungaji kutoka nchi 7 zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki ambazo ni Kenya, Uganda, Sudan Kusini, Tanzania, DR Congo, Burundi na Rwanda.

Akifungua Kongamano hilo, Mkuu wa Wilaya hiyo Sauda Mtondoo amewashukuru Viongozi hao kwa maono yao mazuri ya kuliombea amani na utulivu taifa la Tanzania na chaguzi 2 zitakazofanyika mwaka huu na mwakani.

Amebainisha kuwa Watumishi wa Mungu wana nafasi kubwa sana katika suala zima la kudumishwa amani na utulivu wa nchi, hivyo akawaomba kuendeleza maono hayo kwa nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Bara zima la Afrika.

Aidha amewataka kuendelea kuhubiri amani, upendo na mshikamano na kukemea maovu ili jamii iendelee kuwa na hofu ya Mungu na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ikiwemo uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu.

‘Huwezi kufanya shughuli za kiroho mahali popote kama hakuna amani na utulivu miongoni mwa jamii, na nchi yoyote haiwezi kufanya shughuli za maendeleo kama hakuna amani, umoja na mshikamano miongoni mwa watu wake’, ameeleza.

DC Mtondoo amesisitiza kuwa serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan inaunga mkono kazi nzuri zinazofanywa na Viongozi wa dini na kuahidi kuwa wataendelea kuwapa ushirikiano ili kufanikisha shughuli zao.

Aidha amewapongeza kwa kuanzisha Umoja wao unaohusisha Viongozi wa Makanisa mbalimbali kutoka Mataifa 16 Barani Afrika unaoitwa Leadership Empowerment International Network (LEIN) ikiwemo waumini wao.

Rais wa Umoja huo Bishop Dr. David Makimei kutoka Kenya amesema kuwa LEIN ilianzishwa mwaka 2012 baada ya kufanyika kwa kongamano kama hilo nchini DRC, lengo kuu likiwa kuunganisha nguvu ya utumishi na kudumishwa amani, kwa sasa umoja huo una wanachama kutoka nchi 16.

‘Tunashukuru sana kwa mapokezi mazuri na mkutano wa baraka hapa Tanzania, mwaka 2022 tulienda Congo wakatupokea vizuri, na leo 2024 tupoTanzania, matarajio yetu ni kwenda nchi ya Sudani Kusini mwakani’, ameeleza.

Askfu Eusto Chanangula kutokea Songea, Tanzania, amesema kuwa baada ya kongamano hilo ana amini kila Kiongozi atakuwa ameongeza maarifa na maono zaidi ya kumtumikia Mungu kwa upako wa hali ya juu.

Mchungaji mwenyeji Salome Shimba wa kanisa la International Pentecostal Assemblies of God amebainisha kuwa Viongozi hao pia watashiriki zoezi la uchangiaji damu ili kuokoa maisha ya mama na mtoto na wahanga wa ajali za barabarani.

Rais wa LEIN Bishop Dr. David Makimei (katikati) akiwa na baadhi ya Maskofu na wachungaji kutoka nchi 16 waliohudhuria ufunguzi wa kongamano la mafunzo ya Uongozi na kuombea chaguzi zijazo nchini Tanzania kufanyika kwa amani.
Maaskofu na Wachungaji kutoka mataifa mbalimbali Barani Afrika wanaounda Umoja wa Leadership Empowerment International Network (LEIN) wakiiombea Tanzania na Afrika kuwa na Amani.
Mkuu wa Wilaya ya Igunga Sauda Mtondoo akitoa hotuba ya ufunguzi wa kongamano la mafunzo ya Uongozi, na kuiombea Tanzania kufanya chaguzi zake zijazo za Serikali ya mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa amani, kongamano hilo limeandaliwa na kanisa la International Pentecostal Assemblies Of God-Igunga