Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Maandalizi ya uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu yanayoendelea katika uwanja wa Sabasaba mkoani Njombe yamefikia asilimia 99, ambapo kesho Aprili 2, 2022 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Philip Isdor Mpango anatarajiwa kuzindua mbio hizo zitakazofikia kilele chake Oktoba 14, 2022 mkoani Kagera.
Akizungumza leo mkoani Njombe, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako amesema kuwa baada ya uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2022 vijana sita waliondaliwa kutoka Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar, wataukimbiza Mwenge wa Uhuru katika mikoa 31 na halmashauri 195 nchini kwa siku 195.
“Mwenge wa Uhuru utafanya kazi ya kuhamasisha amani, umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa pamoja na kuhamasisha wananchi kushiriki shughuli za maendeleo katika maeneo yao ambapo ujumbe wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu umezingatia, hoja, na vipaumbele vya Serikali ikiwa ni pamoja na umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 na kauli mbiu ya Mwenge mwaka huu ni Sensa ni Msingi wa Mipango ya Maendeleo: Shiriki kuhesabiwa, tuyafikie Maendeleo ya Taifa”. Alisema Profesa Ndalichako.
Aliongeza kuwa matarajio ya Serikali ni kama yalivyokuwa maono ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye alisema “Sisi tumekwisha uwasha Mwenge wa Uhuru na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, umulike ndani na nje ya mipaka yetu, ulete matumaini pale ambapo hakuna matumaini, ulete upendo mahali penye chuki na heshima mahali palipojaa dharau”
Aidha, Prof. Ndalichako alisema kuwa kuwa Mbio za Mwenge wa Uhuru zitaendelea kuelimisha na kuihamasisha jamii ya Watanzania kuhusu umuhimu na uzingatiaji wa lishe bora, mapambano dhidi ya rushwa, ugonjwa UKIMWI pamoja na mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya na Malaria.
Naye, Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Judica Omary alisema kuwa mkoa huo umefikia asilimia 99 ya maandalizi na sasa wameendelea kuwapokea viongozi mbalimbali wakitaifa watakaoshiriki katika sherehe za uzinduzi wa mbio hizo.
Aliongeza kuwa Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika wilaya sita za mkoa huo ambapo miradi ya afya, elimu, maji na barabara itazinduliwa. Vilevile amewaomba wananchi wote wa Njombe na watanzania kwa ujumla, kujitokeza kwa wingi katika katika uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2022.
More Stories
ITA chatakiwa kutoa mafunzo ya viwango vya juu na kasi ya maendeleo ya Kisayansi
Wagombea CHADEMA wakipewa ridhaa,watakuwa wawazi
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake