Na Iddy Lugendo, Timesmajira Online DSM
IMEELEZWA kuwa idadi ya washiriki katika maonesho ya 47 ya kimataifa ya Biashara maarufu Sabasaba, imeendelea kuongezeka ambapo mpaka sasa kuna jumla ya wafanyabiashara 1317 kutoka ndani na nje ya nchi.
Hayo yameelezwa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Biashara TANTRADE, Fortunatus Mhambe katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo Mei 26,2023 kwenye Ofisi za Taasisi hiyo Jijini Dar es Salaam.
Amesema jumla ya Kampuni 1203 za ndani ya nchi na nyingine 114 kutoka nje ya nchi zitashiriki.
“Nchi 14 zimeomba kushiriki katika maonesho haya ya 47, nchi hizo ni pamoja na China, Umoja wa Falme za nchi za Kiarabu (UAE), Uturuki, Kenya, Ghana, India, Singapore, Syria, Iran, Indonesia, Rwanda, Algeria na Pakistan, “amesema Mhambe.
Akizungumzia uwepo wa Banda la Sabasaba Expo Village kwenye maonesho ya mwaka huu, Katibu Mtendaji wa Taasisi Binafsi Biashara za Madini, Mhandisi, Benjamin Mchwampaka amesema Banda hilo litajumuisha mambo mengi yanayo husika na madini kwa ujumla, tofauti na miaka mingine ambapo kila mdau alikuwa na Banda lake.
Nae Afisa Miradi wa Mfuko unaosaidia Wajasiriamali kutoka Vijijini, Bertha Kageruka, amesema zaidi ya wanawawake 50 Wajasiriamali kutoka mikoa mbalimbali watashiriki maonesho hayo.
Amesema kinamama wengi waliopo vijijini wamethibitisha ushiriki wao, ambapo pia, wamewezeshwa kwa kupewa elimu namna ya kuboresha bidhaa zao.
Kwa upande wake Afisa Mwandamizi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Latiffa Kigoda amesema taasisi yao itashiriki katika maonesho hayo kwa lengo la kuhamasisha wawekezaji katika sekta zote nchini.
Amesema kwa mwaka huu TIC itawakusanya kampuni mbalimbali zinazohusiana na masuala ya uwekezaji ili kuweza kuwahudumia wateja papo kwa papo.
“Mtanzania na wageni wote watakapofika katika Banda la TIC watapata fursa ya kuhudumiwa na upata ausajili wa kampuni, leseni ya biashara, TIN na Huduma nyingine za kibiashara“ amesema Latifa.
More Stories
Kiswaga:Magu imepokea bilioni 143, utekelezaji miradi
Zaidi ya milioni 600 kupeleka umeme Kisiwa cha Ijinga
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini