Na Agnes Alcardo,TimesmajiraOnline, Kilimanjaro
WAZIRI wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, ameanza kutekeleza agizo la Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi,aliyoitaka Wizara hiyo kuhakikisha wanafunzi wa vyuo vikuu katika Mkoa wa Arusha, wanalipwa fedha zao za kujikimu (Boom) ndani ya mwezi huu.
Prof. Mkenda ambaye pia ni mbunge wa Rombo, akizungumza kwenye kikao cha ndani cha Viongozi na Mabalozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Kilimanjaro, mbele ya Katibu Mkuu wa CCM,amesema kuwa Wizara yake imepokea agizo hilo na kwamba watalitekeleza kabla ya mwisho wa mwezi.
“Ndugu Katibu Mkuu jana pale Arusha ulitoa maelekezo kuhusu suala la boom na naomba nitumie nafasi hii kusema kuwa suala hilo tutalifanyia kazi na kabla ya muda uliyotoa wanafunzi wote nchini watalipwa,”amesema.
Aidha, taarifa zilizotolewa hivi punde zinasema kuwa, mara baada ya tamko la Dkt. Nchimbi, fedha hizo tayari zimeanza kuingia kwenye akaunti za wanafunzi.
Mwandishi wa gazeti hili alifanya mahojiano kwa njia ya simu na Mwanafunzi wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii (CBTI) Tengeru, Digna Nasari, ambaye alihudhuria katika mkutano wa hadhara wa Katibu Mkuu wa CCM na kuelezea changamoto hiyo, amesema kuwa baada ya agizo la Katibu Mkuu kutolewa jana Juni 4, 2024 katika mkutano wake wa hadhara uliofanyika Usa River, Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha akiwa anapita akielekea kwenye ziara yake katika Mkoa wa Kilimanjaro limeanza kutekelezwa.
Digna amesema, wanafunzi wa vyuo hivyo walianza kupokea fedha zao za kujikimu Majira ya saa 8 mchana na kusema kuwa wanashukuru kutekelezwa kwa agizo, huku akidai kuwa hali ya kutopata fedha hizo ilidumu kwa muda wa miezi minne na kusababisha baadhi ya wanafunzi kutumia njia zisizohalali kujipatia fedha ya kujikimu.
“Kwa kweli tunashukuru sana na sikuwasilisha suala lile kwa Katibu Mkuu kwa ubaya, kwani hali ya kimaisha kwa wanafunzi ilikuwa ngumu mno kwa miezi minne na wengine walikuwa wanatumia njia wanazojua wao ili wapate pesa na nyumbani huwezi kuomba kwani wanajua unapata Boom hivyo tunaishukuru sana Serikali yetu na chama cha mapinduzi kwa kusikiliza kero za wananchi na kuzifanyia kazi”, amesema Digna.
Ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, hivi sasa inaendelea katika Mkoa wa Kilimanjaro, akiwa ameambatana na Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, CPA Amos Makalla na Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI), Rabia Hamid Abdallah, lengo likiwa kuangalia uhai wa Chama, kusikiliza na kutatua kero za wananchi na kuangalia utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi 2020/2025
Dkt. Nchimbi akiwa eneo la Usa River Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, alitoa maagizo kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhakikisha wanafunzi wa vyuo wanalipwa fedha hizo ifikapo mwisho wa mwezi June.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato