November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Maafisa wa bandari ya Beirut Wawekwa kifungo cha nyumbani Lebanon

Baadhi ya maafisa wa mji wa Beirut wamewekwa katika kifungo cha nyumbani huku wakisubiri uchunguzi kuhusu mlipuko mkubwa wa siku ya Jumanne uliopelekea zaidi ya watu 135 kuuawa Lebanon.

Manal Abdul Samad Najd, Waziri wa Habari wa Lebanon amesema kuwa, kifungo cha nyumbani kitawashirikisha maafisa wote wa bandari, ambao walihusika katika suala la kuhifadhi amoniamu naitreti , wakiilinda na kusimamia usimamizi wake tangu Juni 2014.


Wakati huo huo, Wizara ya Afya ya Lebanon imetangaza kuwa, idadi ya watu waliofariki dunia katika mlipuko huo wa siu ya Jumanne imeongezeka na kufikia wahanga 135 huku waliojeruhiwa wakiwa takriba elfu tano.


Mlipuko huo ulitokea katika ghala nambari 12 la Bandari ya Beirut na kwamba sababu ya moto ni mada za milipuko ambazo zilikuwa zimehifadhiwa hapo.


 Mlipuko huo ulikuwa mkubwa kiasi cha kusikika kilomita nyingi kutoka eneo la tukio. Taarifa zaidi kutoka mji mkuu wa Lebanon Beirut zinasema kuwa, mlipuko huo umesababisha hasara kubwa kwa nyumba za makazi na pia katika idara binafsi na za serikali hasa majengo yaliyokuwa karibu na tukio hilo.


Kwa mujibu wa Rais Michel Aoun tani 2,750 za mada za amoniamu naitreti zinazotumika kwa utengenezaji wa mbolea na mabomu zilikuwa zimehifadhiwa katika bandari ya Beirut kwa muda wa miaka sita bila kuchukuliwa tahadhari za kiusalama.