Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amewataka Maafisa Mawasiliano wa Wizara hiyo na Taasisi zilizo chini yake kutangaza mafanikio ya Sekta ya Elimu ili wananchi waweze kufahamu namna Serikali ilivyowekeza fedha nyingi katika kuboresha mazingira ya utoaji wa elimu nchini.
Waziri Ndalichako ametoa agizo hilo mkoani Morogoro wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha Maafisa hao kilichowashirikisha Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo ambapo amesema mafanikio makubwa katika sekta ya elimu si ya kificho, hivyo ni vyema yakawa yakitolewa kwa wananchi ili waweze kufahamu ni namna gani Serikali yao ilivyowekeza katika kuhakikisha Watanzania wanapata elimu bora.
Amesema ameshuhudia mara nyingi Maafisa Mawasiliano hao wamekuwa wakijielekeza zaidi katika kutangaza matukio ya viongozi wanapokuwa na shughuli mbalimbali katika taasisi zao na baada ya matukio hayo hakuna kinachoendelea. Amewataka Maafisa hao kubadili utaratibu huo na kujikita zaidi katika kutangaza mafanikio makubwa ya uboreshwaji wa mazingira ya kufundishia na kujifunzia.
“Nimefurahi kwamba katika mafunzo haya wakuu wa Taasisi wameshiriki, naamini ushiriki wenu utaleta mabadiliko na kuwa wepesi wa kutoa habari fasaha na kwa wakati. Tuepuke urasimu, yapo mambo yanatokea kwenye vyombo vya habari na mitandao lakini mmekuwa wazito kutoa mrejesho kwa wananchi, ni vizuri kufanyia kazi ili kuepuka mkanganyiko,” amesema Waziri Ndalichako.
Kiongozi huyo amesema kikao kazi hicho kimekuja wakati muafaka ambapo nchi inaelekea kuadhimisha miaka ya 60 ya uhuru na kwamba katika sekta ya elimu kuna mafanikio mengi ambayo yanaweza kuandikwa na kutangazwa pamoja na kuunga mkono juhudi hizo za Serikali kwa nguvu zote.
Akizungumza katika kikao hicho Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe amesema lengo la kikao kazi hicho ni kutathmini utekelezaji wa majukumu ya Mawasiliano katika Wizara na Taasisi zilizo chini yake, kupanga mikakati ya pamoja ya kuboresha utendaji kazi kimkakati pamoja na kupata mafunzo yanayoendana na kada hiyo kutokana na mabadiliko ya kisayansi, kiteknolojia, kisiasa, kijamii na kiuchumi ili kuendelea kuboresha utendaji kazi kimkakati.
Prof. Mdoe ametoa rai kwa maafisa hao kuendelea kufanya kazi kwa karibu na vyombo vya habari ili kuendelea kutangaza mafanikio ya Sekta ya elimu.
Akizungumza kwa niaba ya Viongozi wa Taasisi walioshiriki kikao hicho Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia, Dkt. Amosi Nungu amemuahidi Waziri Ndalichako kuwa wataendelea kutangaza mafanikio hayo kwa ukubwa wake ili fedha zinazotolewa na Serikali matokeo yake yaweze kuonekana.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja