March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Maafisa, Askari Uhifadhi TANAPA watakiwa kujiendeleza Kielimu

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

KAMISHNA wa Uhifadhi TANAPA, CPA Musa Nassoro Kuji, amewahimiza Maafisa na Askari wa Uhifadhi waliopo Makao Makuu na Kanda ya Kaskazini kujiendeleza kielimu ili kuongeza ufanisi wa kazi.

Hayo aliyasema leo Julai 16, 2025, katika kikao kilichofanyika Ukumbi wa Kibo, Makao Makuu ya TANAPA.

Kamishna Kuji amesema, elimu huongeza maarifa, ujasiri, na uwezo wa kukabiliana na changamoto za kazi, kuboresha huduma kwa watalii na kuleta ubunifu kazini.

Amesisitiza kuwa, ujuzi zaidi husaidia kutumia mbinu za kisasa katika uhifadhi na kutoa huduma bora kwa wateja, hivyo ni muhimu kwa watumishi kujiendeleza kielimu ili kuongeza weledi na ufanisi.

Hata hivyo, amewapongeza watumishi kwa mchango wao mkubwa kwenye kampeni ya upigaji kura za tuzo za World Travel Awards 2025, ambapo TANAPA ilishinda tuzo 7 kati ya 27 zilizotolewa kwa Tanzania.

Kwa upande wake Naibu Kamishna wa Uhifadhi (Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara), Massana Mwishawa, ameeleza kuwa Maafisa na Askari wako tayari kutekeleza maelekezo ya Kamishna kwa bidii na morali ya hali ya juu.

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Theophilo Alexander, kwa niaba ya watumishi, aliahidi utekelezaji wa majukumu kwa weledi, bidii na ufanisi, sambamba na kujiendeleza kielimu kwa manufaa ya Shirika na Taifa.

Kikao hicho ni sehemu ya ziara za Kamishna wa Uhifadhi katika hifadhi za Taifa kwa lengo la kutoa maelekezo, kufuatilia maendeleo ya shughuli za uhifadhi na utalii, na kuimarisha utendaji wa Shirika.