November 8, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Maadhimisho ya siku ya nyuki kufanyika mkoani Katavi

Na Penina Malundo,timesmajira,Online

WATANZANIA wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho ya siku ya Nyuki duniani ambayo kitaifa yanatarajia kufanyika katika wilaya ya Mpanda Mkoani Katavi,Mei 21, 2022 ili kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu umuhimu wa mdudu nyuki katika maisha ya kila siku ya mwanadamu na mazingira yake

Wito huo umetolewa leo na Waziri wa Maliasili na Utalii nchini, Balozi. Dkt.Pindi Chana kwenye taarifa yake kwa waandishi wa Habari Jijini Dodoma.

Waziri Chana ameeleza chimbuko la maadhimisho haya ni azimio la Baraza la Umoja wa Mataifa ,Desemba 20,2017 lililoazimia kuwa Mei,20 ya kila mwaka, kuwa ni siku ya nyuki duniani, kwa lengo kuu la kutambua mchango wa mdudu huyu katika kukuza usalama wa chakula na uhifadhi wa mazingira duniani.

“Kufuatia azimio hilo, kila nchi inajukumu la kuadhimisha siku hiyo kuendana na mazingira yake, ili kuendelea kujenga uelewa kwa jamiii juu ya umuhimu wa mdudu nyuki. Na hii ndiyo sababu, sisi kama nchi, tunaungana na dunia kufanya maadhimisho haya kwa mara ya tatu tangu yalipoanzishwa miaka mitano iliyopita,”amesema Waziri Chana

Akitaja manufaa ya mdudu Nyuki, Waziri Chana amesema ni pamoja na chakula na dawa, kujipatia fedha za ndani na kigeni, ajiri zaidi ya watu milioni 2 katika mnyororo mzima wa thamani itokanayo na sekta ya ufugaji wa Nyuki.

“Wizara ina mikakati ya kuhakikisha sekta hii inaajiri zaidi ya watu milioni 2.5 ifikapo 2031. Aidha, manufaa yatokanayo na nyuki ni mengi zaidi ya ajira, kwani hata chakula tunachokula nyuki ni sehemu ya wachavushaji wakubwa, na hivyo kutuhakikishia upatikanaji wa chakula”. Ameongeza Waziri Chana

Kauli mbiu ya mwaka huu wa 2022 ni “Nyuki wamehusika: Harakati za kujikwamua upya zisisahau nyuki” (Bee engaged: Build back better for bees). Kauli mbiu hii imekuja kufuatia changamoto ambayo dunia inaendelea kuipitia ya UVIKO 19, na nyuki wamesaidia kwenye mapambani dhidi ya janga hili kwa kuimarisha kinga za miili ya watu.

Pamoja na uwepo wa kaulimbiu hiyo ya kidunia, kaulimbiu ya kitaifa kwa mwaka huu wa 2022, nayo inasema “NYUKI NI UCHUMI: TUWALINDE NA KUHIFADHI MAZINGIRA YAO”. Kaulimbiu hii inaendana na ile ya kidunia kwa kuendelea kuhamasisha wadau kuendelea kutambua umuhimu wa kuwalinda na kuwahifadhi nyuki ili kupata manufaa ya kiuchumi na kiafya.