November 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii kupima ubora wa majibu kwa wagonjwa ya binadamu

Na Mwandishi Maalumu, TimesMajira Online – Dar Es Salaam

Serikali kupitia Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii imeanza kuandaa sampuli kwa ajili ya kupima ubora wa majibu yanayopimwa kwa magonjwa ili kuweza kuweza kutoa huduma za matibabu sahii kupitia watoa huduma za afya nchini.

Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi wa maabara hiyo Bw. Medard Beyanga wakati akiongea na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Afya Bi. Catherine Sungura alipotembelea maabara hiyo jijini Dar es Salaam.

Beyanga amesema kuwa maabara hiyo yenye ithibati ya Viwango vya Kimatifa iliyotolewa mwaka 2014 (ISO 15189) vya kupima magonjwa ya binadamu imeanza kutengeneza sampuli za upimaji ubora wa huduma za maabara na kuzipeleka katika maabara za Mikoa ambapo maabara zilizopo mikoani hupima sampuli hizo na majibu yake hurudishwa Maabara ya Taifa na kupima ubora wa majibu yaliyopimwa.

“Tunapanua huduma zetu za maabara, tunataka kuhakikisha mgonjwa anayepimwa pote nchini wanakuwa na majibu sahihi, mgonjwa akipimwa kipimo mkoa mmoja akienda kupimwa mkoa mwingine majibu yafanane ili kuwasaidia watoa huduma katika kutoa huduma bora za matibabu”.Amesema Beyanga.

Amesema wanaishukuru Serikali kwa kuwapatia Mashine na vifaa vya kisasa vyenye uwezo wa kupima magonjwa tofauti tofauti na hivyo hakutakuwa haja ya kupeleka sampuli nje ya nchi kama ilivyokuwa hapo awali.

“Maabara hii kwa sasa ndio maabara ya Rufaa hapa nchini, hivyo tunashukuru Serikali kwa kutupatia mashine na vifaa vya kisasa vyenye uwezo ambapo tunaweza kuondoa rufaa za sampuli zilizokuwa zikienda nje ya nchi na hivyo kuipunguzia Serikali gharama na kwa sasa tunaendelea kuwajengea uwezo wataalam wetu” .

Kwa upande wa upimaji wa UVIKO-19 amesema hivi sasa wamekuwa na mafanikio makubwa na kuweza kuwarahisishia wananchi pamoja na wasafiri huduma za upimaji UVIKO-19 kwani wameweza kugatua maabara hizo kutoka vituo viwili Julai mwaka 2021 na sasa wameongeza vituo kwenye Mikoa ya Mwanza, Arusha, Mbeya, Kagera, Dodoma,Kigoma pamoja na Ngorongoro kwa ajili ya kuwapunguzia usumbufu watalii na hivi sasa wanatarajia kupeleka katika Mikoa ya Mtwara na Lindi.

Aidha, Beyanga amesema kuwa kutokana na mashine za kisasa walivyopatiwa na Serikali wameweza kupata mafanikio kwa kuweza kupunguza muda wa kupima na kupata majibu kwa kuweza kupima sampuli takribani 500 ndani ya saa tano hivyo imesaidia kuondoa malalamiko na hivyo kufanya majibu kutolewa ndani ya saa 24.

“Tumefanya mafunzo ya upimaji kwa wataalam nchi nzima ili kuhakikisha wanakuwa na uwezo wa kuchukua sampuli na upimaji kwa ufasaha kulingana na utaratibu na miongozo lengo ni kufikia Hospitali zote za Rufaa za Mikoa kupima sampuli” Aliongeza Beyanga

Licha ya hayo Mkurugenzi huyo amesema kuwa Maabara hiyo pia ina uwezo wa kupima magonjwa mengine ya mlipuko ambayo kama nchi inafanyia ufuatiliaji ikiwemo Ugonjwa wa Mapafu, Kipindupindu, Homa ya Mapafu,Surua Rubela na mengineyo.

Hata hivyo amesema hivi sasa wapo katika maandalizi ya kupima magonjwa yasiyo ambukiza na kuongeza kuwa wana uwezo wa kufanya uchambuzi wa vinasaba wa ugonjwa wa UVIKO-19 na hivi karibuni wanategemea kuanza kufanya uchunguzi wa vinasaba vya magonjwa ya Kansa pamoja na kutengenza sampuli zitakazokuwa wanazisambaza kwenye Hospitali za Mikoa na binafsi ili waweze kupima ubora utakaoweza kuwasaidia watoa huduma kutoa matibabu sahihi.

Kaimu Mkurugenzi wa Maabara hiyo Bw. Medard Beyanga akiongea na Bi. Catherine Sungura, kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini (hayupo pichani) wakati wa mahojiano kuhusu maabara hiyo ilivyopiga hatua kutokana na maboresho makubwa ikiwemo vifaa vya kisasa walivyopewa na Serikali.
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Bi. Sungura akiangalia vifaa vya kisasa vilivyoko kwenye maabara hiyo
Wataalamu wa maabara wakiwajibika ikiwa ni pamoja na upokeaji wa sampuli na upimaji  katika maabara hiyo.
Kaimu Mkurugenzi wa maabara hiyo Bw. Beyanga  akielezea moja ya mashine ya kisasa inavyofanya kazi na yenye uwezo mkubwa na hivyo kupata mafanikio katika kupima sampuli za magonjwa kwa muda mfupi tofauti na awali.
Mtaalamu wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii akiendelea na kazi katika maabara hiyo