December 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Lwanhima,waanza kupata maji

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Mradi wa maji wa matokeo ya haraka wa Lwahima-Buhongwa,jijini Mwanza,umefikia asilimia 90, na umeanza kutatua changamoto ya maji kwa baadhi ya wananchi wa mitaa ya maeneo hayo kutoka saa tatu za kutafuta maji mpaka dakika 5 hadi 30.

Hayo yamebainishwa Septemba 24,2024 na baadhi ya wananchi mitaa ya Semba,Sahwa ya Juu na Chini,Kagera Kata ya Lwahima,wakati Mbunge wa Jimbo la Nyamagana Stanislaus Mabula alivyoungana na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza(MWAUWASA),katika ziara ya ‘mtaa kwa mtaa’,sema usikike,’.

Rosemary Bernard, kutoka mtaa wa Semba,ameeleza kuwa,walikuwa wananunua ndoo ya maji ya lita 20 kwa sh.500 kutoka kwa wauzaji wanaotembeza maji mitaani.Wakati mwingine wanaenda kuchota maji kwenye mito midogo au chemuchemu,ambayo inatoa maji kidogo na wanatumia bakuli kuchota maji,hali inayochukia saa tatu hadi nne, kujaza ndoo moja ya lita 20.

“Licha ya kwamba kwa sasa maji bado hayajafika kwa wananchi wote,baadhi yetu tumepata unafuu,baada ya maji kuanza kutoka katika gati hili la hapa Semba, hivyo tunatumia dakika 5 hadi 30,kupata maji na kwa bei ya sh.50 kwa ndoo ya lita 20,tofauti na awali wauzaji walituuzi ndoo ya lita 20 kwa sh.500,”ameeleza Rosemary.

Mary Juma,kutoka mtaa wa Sahwa ya Chini, amesema,”Hali hii imetusaidia kiuchumi, kwani katika sh.500 ambayo tulikuwa tunapata maji ndoo moja ya lita 20,kwa sasa tunapata ndoo 10 sawa na lita 200 kwa sh.500.Pia uchumi wetu utaimarika kutokana na kutumia muda mfupi kufanya shughuli za maendeleo, tofauti na awali tukitumia muda mrefu kutafuta maji,ambayo kimsingi ni uhai,”.

“Licha ya jitihada ambazo serikali imefanya za kutatua changamoto ya maji.Naomba ituangalie katika maeneo ambayo hatujapata kwa kuboresha mabomba na wasambaze maji ili yatufikie wananchi wote,” amesema Anitha Peter Mkazi wa Sahwa ya Juu.

Diwani wa Kata ya Lwahima,Marco Swalala,amesema kwa sasa kati ya mitaa 18, mitaa 8 imeweza kupata maji ingawa ni kwa uchache ikiwemo Sahwa,Semba,Kageye, Lwahima Magharibi,Maliza na Ihushi.Hivyo MWAUWASA,pamoja na kazi inayofanya iongeze juhudi na kusambaza mabomba, ili mitaa iliobaki wananchi waweze kufikiwa na huduma ya maji.

Mkurugenzi wa Usambazaji Maji wa MWAUWASA, Mhandisi Robert Lupoja,ameeleza kuwa, utekelezaji wa mradi huo wa dharura, umefikia asilimia 90,na baadhi ya watu wameanza kupata maji.Ambapo kwa kipindi hiki cha majaribio, wanasukuma maji kuanzia saa 1 asubuhi hadi saa 12 jioni,huku kilichobaki ni kufanya maunganisho ndani ya wiki hii, maeneo ya jirani ili watu wote wapate maji.

Sanjari na hayo ameeleza kuwa kupitia mapato ya ndani ya mamlaka hiyo,wamesanifu mradi wa milioni 600,ambao watalaza bomba renye urefu wa kilomita 15,lenye inchi,6,4 na 3.Ambao pia utaunganisha mfumo ambao kwa sasa hivi maji hayaingii kutoka tenki la Kishiri.

“Mradi huu tumepanga kutekeleza katika mwaka wa fedha 2024/2025,awamu ya kwanza tutaweka bomba kubwa ambalo tayari mabomba yake yapo katika hatua ununuzi, na tunategemea kabla ya Desemba mwaka huu mradi huo utakuwa umekamilika.Awamu ya pili ni ulazaji wa mtandao wa mabomba madogo madogo,utafanyika Januari mpaka Juni,2025,lengo ni kuhakikisha maeneo yote yanapata maji saa 24,” amesema Lupoja.

Kaimu Mkurugenzi MWAUWASA,Neli Msuya, ameeleza kuwa wanaendelea na majaribio ya kutoa maji katika mradi huo wa dharura kutoka Sahwa kwenda Buhongwa.Ambapo maelekezo ya Serikali kwenye chanzo cha maji,na maeneo mabomba yanapopita lazima utoe huduma kwa wananchi,

“Tunaendelea na uboreshaji wa mfumo wetu na kuzindua yale maeneo ambayo yalikuwa hayapati maji,mfano hiki kioski(kilichopo mtaà wa Kagera),miaka mitano kilikuwa hakipati maji,lakini sasa kinatoa maji,tumepita katika vioski vingine sita ambavyo tumevifufua na sasa vinatoa maji,”amesema Neli na kuongeza:

“Lakini yapo maeneo mengine ambayo hayapati hata haya maji ya vioski,tupo kazini tunafanya kazi mchana na usiku, hatuwezi kufikia wote mara moja, tunakwenda kwa awamu tunaendelea na majaribio na usambazaji wa maji,”.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Nyamagana Stanislaus Mabula,amewahikikishia wananchi wa maeneo hayo kuwa maji hayo yataendelea kutoka, na huo ni mwanzo mpaka watakapo hakikisha kila mtu anafungua maji nyumbani kwake.

“Mradi huu ukikamilika kwa asilimia 100, utakuwa na vioski vingi vya kuchota maji ili watu muweze kupata maji, wakati tukisubili mradi mkubwa wa bilioni zaidi ya 40 kukamilika katika kipindi cha miezi 18,”ameeleza Mabula na kuongeza:

“Bei elekezi ya maji katika vioski hivyo ni sh.50 kwa ndoo ya lita 20, huku akiwataka wale watu wanazouza maji kwenye madumu mtaani kushusha bei ya maji na siyo sh.500 kama ilivyo sasa,kwani wao wanayapata kwa bei nafuu,”.