December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Luteni Mwambashi aipongeza RUWASA

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online, Tanga

KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2021, Luteni Josephine Mwambashi amesema amefurahishwa na uwajibikaji wa Wakala Usambazaji Maji Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Tanga kwa namna walivyotekeleza miradi yao kwa viwango vya juu huku akiwataka wahakikishe vijiji vyote vinapata huduma hiyo muhimu ya maji safi na salama.

Luteni Josephine ameyasema hayo wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru ambao uliweka jiwe la msingi pamoja uzinduzi wa miradi katika wilaya za Pangani na Muheza.

Amesema, RUWASA Mkoa wa Tanga imejitahidi kutekeleza maelekezo ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji kwa kiwango kikubwa.

Akiwa wilayani Muheza aliitaka RUWASA kuhakikisha inamalizia miradi mbalimbali iliyoanza na ile iliyopo kwenye bajeti ijayo.

“Nimefurahishwa hasa huu mradi mkubwa wa Umba, mradi huu unakwenda kumtua mama ndoo kichwani, endeleeni na kazi nzuri, lakini mhakikishe bajeti inayokuja vijiji vyote vinaunganishiwa na huduma ya maji,”amesema Josephine.

“Tumeona ushirikiano wa mzuri wa viongozi katika wilaya ya Muheza na ndio unapelekea kuongeza kasi ya maendeleo mbalimbali nchini hivi ndivyo tunavyataka sasa,”amebainisha Luteni Mwambashi.

Kwa upande wake Meneja wa Ruwasa Mkoa Tanga, Upendo Lugongo amesema kuwa, katika bajeti yao ya mwaka 2021 wametenga bajeti kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi wa maji wa Ngomeni kwa sababu tenki wanalotumia kuchukua maji ni ndilo lenye mradi wa maji la Umba.

Waziri wa Maji, Juma Aweso ametoa rai kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge 2021 kuipitia na kukagua miradi yote ya maji ili ripoti yake iweze kumsaidia kuongeza ufanisi

Amesema, mradi huo mradi huo utakwenda kuhudumia kijiji cha jirani kwa kuunganisha mtandao wa mabomba.

Mwenge wa Uhuru ukiwa wilayani Mkinga umeifikia jumla ya miradi 10 yenye thamani ya kiasi cha bilioni 1.4 huku ikiwa imezinduliwa, kukaguliwa na kuweka jiwe la msingi wilayani humo.