December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Luteni Mwambashi ahamasisha upandaji miti

Na Hadija Bagasha Tanga,TimesMajira Online

KATIKA kuelekea wiki ya mazingira Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2021, Luteni Josephine Mwambashi ameiasa jamii kuendelea kupanda miti katika maeneo yao ili kuendelea kupata hewa safi na hatimaye kukabiliana na mmomonyoko wa udongo.

Kiongozi huyo ameyasema hayo wakati alipofika kata ya Malindi wilayani Lushoto mkoani Tanga na kupanda mti mmoja kama ishara ya kurejesha uoto wa asili.

Luteni Mwambashi amesema kuwa, jamii inapaswa kuhakikisha wanajikita katika utaratibu wa upandaji wa miti hasa katika maeneo ya Mkoa wa Tanga yaliyojaaliwa neema ya mvua jambo litakaloongeza kasi ya ukuaji.

“Upandaji miti ni namna bora ya kurudisha uoto wa asili uliyoharibika lakini pia ukataji miti kiholela kusababisha kutokea kwa jangwa na ukame hivyo niwasihi ndugu wananchi muendelee kupanda miti kwa wingi, “amesisitiza Luteni Mwambashi.

Amesema, upandaji wa miti ni njia mojawapo itakayoweza kusaidia kuendelea kupata hewa safi lakini pia itasaidia kuondoa mmomonyoko hasa katika maeneo ya barabara.

Luteni Mwambashi amewaasa waendelee kutunza vyanzo vya maji pamoja na kuzuia shughuli za kibinadamu katika vyanzo hivyo.

Ukiwa wilayani Lushoto Mkoani Tanga Mwenge wa Uhuru ulikagua miradi 12 yenye thamani ya shilingi bilioni 2.188 ikiwemo mradi wa maji, afya, elimu, barabara, na mradi wa vijana wajasiriamali.

Ambapo katika, miradi hiyo imepitiwa kwajili ya kukaguliwa, kuzinduliwa na kuwekewa jiwe la msingi wilayani Lushoto mkoani Tanga.