Na Penina Malundo,Timesmajira
MNADHIMU Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, Luteni Jenerali Salum Haji Othmani, amesaini mkataba wa utekelezaji wa mradi wa kupima fursa kwa wanawake katika Operation za Ulinzi wa Amani, mradi huo unafadhiliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Elsie Initiative Fund kupitia UN Women Tanzania.
Utekelezaji wa mradi huo wa kutathmini mapungufu na vikwazo katika ushiriki wa wanawake kwenye operesheni za kulinda amani umeanza rasmi baada ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kusaini mkataba wa mwaka mmoja na taasisi tatu muhimu zitakazotekeleza mradi huo.
Akizungumza baada ya utiaji saini huo, Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Luteni Jenerali Salum alisema tathmini hiyo itatoa mapendekezo yatakayosaidia kuimarisha sera, mifumo ya kiutendaji na mazingira wezeshi ili kuhakikisha wanawake wanapata zaidi nafasi za uongozi katika misheni za kulinda amani.
Amesisitiza kuwa mradi huo pia utafanya tathmini na kuangalia michakato ya uchaguzi na uteuzi ili kubaini kama kuna mazingira yanayokwamisha wanawake kushiriki ipasavyo katika oparesheni hizo za ulinzi wa amani.

“Ushirikiano huu wa hizi taasisi unaonesha dhamira ya dhati ya Tanzania kutekeleza ajenda ya Wanawake, amani na usalama,” amesema Luteni Jenerali Othumani.
Hata hivyo alisema Luteni Jenerali Othumani kuwa ripoti ya mwisho ya tathmini ya mradi huo inatarajiwa kutolewa Septemba mwaka huu.

Kwa mujibu wa mkataba huo, mradi huo unaofahamika kama Measuring Opportunities for Women in Peace Operations (MOWIP) unafadhiliwa na Mfuko wa Elsie Initiative kupitia UN Women Tanzania, ukiwa na lengo la kubaini vikwazo vya kimfumo, kitamaduni, kiutendaji na kiusalama vinavyozuia ajira, kubaki kazini, kutumwa kazini na uongozi wa wanawake katika vyombo vya ulinzi na usalama.
Mradi huo unaendana na Mpango wa Kitaifa wa Wanawake, Amani na Usalama (2025–2029) na unatarajiwa kuimarisha mifumo ya kitaifa ya utafiti na takwimu sambamba na kukuza ushirikiano kati ya sekta za ulinzi, taaluma na taasisi za masuala ya kijinsia.
Miongoni mwa Taasisi hizo ambazo zitatekeleza mradi huo ni Shirika la Umoja wa Mataifa la UN Women Tanzania, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).

Naye Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani Tanzania (TPTC), Brigedia Jenerali George Itang’are amesema mkataba huo uliyosainiwa utatumika katika kutekeleza mradi huo wa mwaka mmoja huku maeneo muhimu yatakayoangaliwa ni sifa zinazotumika kupata wanawake katika oparesheni za ulinzi wa amani kama si kikwazo kwao kushiriki.
Amesema pia mradi huo utaanagalia kama mifumo inayotumika ya uteuzi je inatoa nafasi sawa ya wanawake kushiriki katika opareshini hizo pamoja na kuangalia mambo ya kifamilia yanayowakwamisha wanawake kushiriki katika masuala ya ulinzi wa amani.

“Tutaangalia pia ujuzi pamoja na uzoefu wa wanawake waliowahi kushiriki katika shughuli mbalimbali za ulinzi wa amani kwa kukusanya maoni kutoka kwao na jamii zinazowazunguka, lengo ni kubaini iwapo mrejesho kutoka kwenye jamii unachochea au unazuia ushiriki wao,” amesema
Hata hivyo amesema kuwa watafiti katika mradi huo wanatarajia kubaini mifano bora ya utekelezaji pamoja na kuandaa mapendekezo yatakayoimarisha ushiriki wenye tija wa wanawake katika shughuli mbalimbali za ulinzi wa amani.

Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa UN Women nchini, Katherine Gifford, ameipongeza Tanzania kwa kuanza rasmi kutekeleza mradi huo, akieleza kuwa ni hatua muhimu katika kuimarisha ushirikishwaji wa kijinsia katika juhudi za nchi za kudumisha amani na usalama.
Gifford amesema kuwa mradi huo ni mfano mzuri wa ubia uliojengwa juu ya misingi ya heshima, utaalamu na dhamira ya pamoja huku akisisitiza kuwa mchango wa muda mrefu wa Tanzania katika operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika, pamoja na juhudi za kuongeza ushiriki wa wanawake katika misheni hizo.

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina